Na Saidi Lufune, Dodoma
KATIKA kukabiliana na Wanyamapori wakali na waharibifu kwa wananchi wanaozunguka hifadhi na mapori tengefu Serikali imeendelea kubuni na kutumia teknolojia mseto ikiwemo uzio wa umeme ili kuimarisha ulinzi na usalama kwa wananchi dhidi ya Tembo wanaoingia katika makazi na mashamba.
Hayo yamesemwa Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), katika kikao cha 5 Mkutano wa Pili wa Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati akijibu swali la Mbunge wa Kisesa Mhe. Musa Godfrey Mbuga (Mb), aliyetaka kufahamu aina ya mbinu mpya zinazotumiwa ili kukabiliana na tembo katika vijiji vya Ng’hanga, Mwambongo, Matale, Longalonhinga, Sakata, Nyanza na Banhya.
“Serikali kupitia wadau wa uhifadhi ina mpango wa kuweka uzio wa umeme (electrified fence) kuzunguka mpaka wa hifadhi ya pori la akiba la Maswa kwa upande wa magharibi unaopakana na makazi ya wananchi utakaozuia tembo kutoka nje ya hifadhi na kuleta madhara kwa wananchi.” Alisema Mhe. Chande
Katika hatua nyingine Mhe. Chande ameongeza kuwa, Serikali imeandaa mkakati mpya wa kitaifa wa kusimamia utatuzi wa migongano baina ya binadamu na wanyamapori 2025/26 hadi 2035/36 kwa ushirikiano na wizara za kisekta ikiwemo OWM-TAMISEMI, Maliasili na Utalii, Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi chini ya uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu ili kufanikisha kupunguza changamoto hiyo kwa pamoja na kwa ufanisi mkubw
Ushirikiano kati ya Wizara ya Maliasili na Utalii na Wizara nyingine za kisekta kutafuta suluhu ya migogoro baina ya binadamu na wanyamapori wakali na waharibifu itasaidia nchi kuwa na mfumo thabiti ulioratibiwa na kuzingatia maslahi ya wananchi kwenye makazi yao na maendeleo endelevu ya uchumi wa Taifa.


.jpeg)


No comments:
Post a Comment