MKUU wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga Peter Masindi, amesema kulipa kodi ni muhimu sana kwa maendeleo ya Taifa kwani kupitia Kodi Serikali imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika jamii.
Ameyasema hayo hivi karibuni wakati alipotembelewa na Maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Ofisini kwake Wilayani Kishapu kwa lengo la kumjuulisha juu ya uwepo wa zoezi la elimu ya kodi mlango kwa mlango wilayani humo.
Masindi, amesema kupitia kodi Serikali imeendelea kuimarisha miundombinu mbalimbali na hatimae kuboresha huduma za kijamii.
"Ukilipa kodi ndio unajenga barabara, shule, hospitali, unachangia uwepo wa huduma za maji na miradi ya kimkakati kama Treni ya Mwendokasi (SGR)" amesema Masindi.
Aidha, ameipongeza TRA kwa kuendelea kukusanya kodi kwa mafanikio huku akitolea mfano wa kuvunja kwa rekodi ya makusanyo kwa kila mwezi kwa TRA Shinyanga na maeneo mbalimbali nchini Tanzania.
Mbali na hayo, amewapongeza wafanyabiashara wa Kishapu kwa kuendelea kulipa kodi kwa hiari huku akisisitiza TRA kuendelea na urasimishaji wa Wafanyabiashara kwani utaongeza wingi wa mapato na hatimae kuboresha huduma za kijamii kadri zinavyohitajika.
Pamoja na hayo, ameiomba TRA kuweka Ofisi ya Huduma za Kikodi Wilayani Kishapu kwani kukosekana kwa Ofisi katika Wilaya hiyo kunasababisha changamoto kwa walipakodi.
"Tunahitaji Ofisi ifunguliwe (Kishapu) kwa ajili ya kuwarahisishia walipakodi kuendelea kulipa kodi kwa hiari, kwani kwa sasa wananchi wanatembea umbali mrefu kwa ajili ya kuzifuata huduma za kikodi" amesema Mhe. Masindi.
Kwa Upande wake, Afisa Msimamizi wa Kodi mkoa wa Shinyanga Semeni Mbegi kwa niaba ya Kiongozi wa timu hiyo amesema katika kipindi cha takriban wiki moja wameweza kutembelea zaidi ya wafanyabiashara 2000 kwa kuwapatia elimu na kusikilza changamoto zao.
Amefafanua kuwa katika zoezi hilo wamebaini mambo mbalimbali ikiwemo baadhi ya wafanyabiashara kufanya biashara bila ya kujisajili TRA, baadhi ya wafanyabiashara biashara zao bado hawajakadiriwa, na baadhi yao hawatumii mashine za EFD ipasavyo.
Semeni ametoa wito kwa wafanyabiashara kuhakikisha wanasajili biashara zao, wanakadiriwa na kulipa kodi ya awamu kwa wakati ili kuiwezesha Serikali kukamilisha miradi ya maendeleo kwa wakati.



.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
No comments:
Post a Comment