HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, February 9, 2026

Serikali yazindua Sera ya Taifa ya Kinga ya Jamii na ‘Hifadhi Scheme’ kwa Waliojiajiri


Serikali yazindua Sera ya Taifa ya Kinga ya Jamii na ‘Hifadhi Scheme’ kwa Waliojiajiri

Na MWANDISHI WETU, 

ARUSHA. Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano imezindua Sera ya Taifa ya Kinga ya Jamii pamoja na Mpango wa Hifadhi ya Jamii kwa Wananchi Waliojiajiri ‘Hifadhi Scheme’ hatua inayolenga kupanua wigo wa hifadhi ya jamii na kuongeza ushirikishwaji wa wananchi katika mifumo ya kinga ya kijamii.

Uzinduzi huo umefanyika Februari 9, 2026 katika mkutano wa wadau wa sekta ya kinga ya jamii uliofanyika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC), ukiongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Sangu alisema sera hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kuhakikisha wananchi wanapata huduma jumuishi za hifadhi ya jamii. Aliongeza kuwa tangu 2018, Serikali imefanya maboresho ikiwemo kuunganisha Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na kubaki na NSSF na PSSSF ili kuongeza ufanisi wa huduma na ulipaji wa mafao.

Mhe. Sangu alisema maboresho hayo yameongeza idadi ya wanachama. NSSF imeongezeka kutoka wanachama 808,935 mwaka 2020 hadi zaidi ya wanachama 2,213,659 mwaka 2025, huku PSSSF ikiongezeka kutoka 697,677 hadi 899,948. Aidha, thamani ya uwekezaji wa Mifuko imeongezeka kutoka shilingi trilioni 9.36 hadi trilioni 20.14, na jumla ya thamani ya Mifuko kufikia trilioni 24.20.

Kuhusu mpango wa Hifadhi Scheme, alisema hadi Desemba 2025 zaidi ya wanachama 500,000 kutoka makundi mbalimbali yakiwemo wakulima, wafugaji, wavuvi na wajasiriamali wamejiunga, huku lengo likiwa kufikia wanachama milioni 5.5 ifikapo Juni 2031.

Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Mary Maganga, alisema Serikali imeipa NSSF jukumu la kupanua wigo wa hifadhi ya jamii kwa wananchi waliojiajiri ili kuhakikisha sera mpya inaleta matokeo yanayotarajiwa.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba, alisema Mfuko unaendelea kuboresha utoaji wa huduma, kuongeza uandikishaji wa wanachama wapya, na kupanua wigo wa uwekezaji ndani na nje ya nchi, ikiwemo nchi za SADC na Afrika Mashariki.

Bw. Mshomba alisema Mfuko umepata mafanikio makubwa katika Serikali ya awamu ya sita ambapo thamani ya NSSF imeongezeka kutoka trilioni 4.8 mwaka 2021 hadi trilioni 10.4 Desemba 2025, na kuwa imepata ziada kwa miaka minne mfululizo kuanzia 2021 hadi mwaka wa fedha 2024/25, ikivuka lengo la ziada ya shilingi trilioni moja.

Akizungumzia ukusanyaji wa michango, Bw. Mshomba alisema Mfuko umeendelea kuvuka malengo, ambapo mwaka wa fedha 2023/24 ulifikia zaidi ya shilingi trilioni mbili, huku mwaka 2024/25 makusanyo yakizidi trilioni 2.4 na kwamba katika kipindi cha miaka mitano mfululizo kuanzia 2020 hadi 2025, NSSF imefanikiwa kuvuka lengo la kukusanya angalau shilingi trilioni moja kwa mwaka. 

Bw. Mshomba aliongeza kuwa mafanikio hayo yamechangiwa na juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. NSSF ina zaidi ya wanachama milioni 2.3 na imejikita kuboresha huduma kupitia TEHAMA na mpango wa miaka mitano unaolenga kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa 2050 na Ilani ya Uchaguzi ya CCM. 



No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad