HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, February 12, 2026

Serikali Kujipanga Kutumia Akili Mnemba Kuboresha Huduma kwa Umma

Na Mwandishi Wetu

NAIBU Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Xavier Daudi, amesema Serikali imejipanga kikamilifu kutumia Teknolojia ya Akili Mnemba (Artificial Intelligence – AI) ili kuongeza ufanisi, kasi na ubora wa utoaji huduma kwa wananchi, kufuatia mabadiliko makubwa ya kidunia katika sekta ya teknolojia.

Daudi aliyasema hayo jijini Dar es Salaam leo, Februari 12, 2026, wakati akifungua mdahalo kuhusu matumizi ya Akili Mnemba (AI) katika kuboresha huduma kwa umma, ulioandaliwa na Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC).

Alisema kuwa licha ya Serikali kuendelea kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika miaka ya hivi karibuni, kasi ya ukuaji wa teknolojia ya Akili Mnemba imeleta mazingira mapya yenye changamoto na fursa katika utumishi wa umma, hivyo kuna umuhimu wa kuendana na mabadiliko hayo.

“Ni dhahiri kuwa mabadiliko ni makubwa katika mazingira na kasi ya ukuaji wa teknolojia. Hatuwezi kubaki nyuma wakati dunia inakwenda kwa kasi. Nasi Serikalini tunapaswa kutumia teknolojia ya akili mnemba kuhakikisha wananchi wanafaidika na huduma zinazotolewa kwa haraka na kwa ufanisi zaidi,” alisema Daudi.

Alieleza kuwa matumizi ya teknolojia hiyo yataisaidia Serikali kupata majawabu sahihi kwa wakati, kutatua changamoto za wananchi kwa ufanisi, na kuwafikia kwa wakati muafaka.

Aidha, alisisitiza kuwa Serikali haijakaa kimya katika suala hilo, bali tayari imeanza kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha mifumo ya utoaji huduma kwa kutumia teknolojia za kisasa. Alitolea mfano eneo la ajira, ambapo mifumo ya kidijitali imeanza kutumika kuboresha mchakato huo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC), Dkt. Ernest Mabonesho, alisema matumizi ya Akili Mnemba katika utumishi wa umma ni hatua muhimu itakayorahisisha utoaji wa huduma na kuongeza ufanisi kwa watumishi.

“Kazi yetu kubwa ni kutoa mafunzo kwa watumishi wa umma, hasa katika mambo mapya yanayoibuka. Utumishi wa umma unabadilika,” alisema Dkt. Mabonesho.

Alibainisha kuwa ingawa Akili Mnemba ni dhana mpya katika utumishi wa umma, ni teknolojia isiyoweza kuepukika.

“Hii ni teknolojia ambayo inatulazimisha tuanze kuitumia kwa sababu inaleta wepesi katika utoaji wa huduma kwa wananchi, pamoja na kuongeza uwazi na ufanisi,” aliongeza.

Naye mshiriki wa mdahalo huo, Mahyolo Kalokola, alisema mjadala huo umemfungua macho kuhusu fursa zilizopo katika matumizi ya Akili Mnemba.





 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad