Na Mwandishi Wetu, Manyara.
SERIKALI imeanza utekelezaji wa mradi mkubwa wa kusambaza umeme katika vitongoji 267 vya Mkoa wa Manyara kwa gharama ya Shilingi bilioni 45.8 kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya umeme na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Akizungumza wakati wa hafla ya kumtambulisha mkandarasi wa mradi huo, mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Herini Mhina, amesema mkataba wa utekelezaji wa mradi huo ni wa miaka mitatu na utatekelezwa katika halmashauri zote za Mkoa wa Manyara.
Mhandisi Mhina amesema mradi huo unalenga kufikisha huduma ya umeme katika vitongoji ambavyo bado havijafikiwa, hatua itakayosaidia kuboresha maisha ya wananchi, kukuza shughuli za kiuchumi pamoja na kuimarisha upatikanaji wa huduma za kijamii kama afya na elimu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga, amewaagiza Wakuu wa Wilaya zote za mkoa huo kutoa ushirikiano wa karibu kwa mkandarasi ili kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa.
Mhe. Sendiga pia amesisitiza umuhimu wa viongozi kutoa elimu kwa wananchi kuhusu utekelezaji wa mradi huo, akieleza kuwa mradi wa kusambaza umeme hauna fidia, hivyo ni muhimu wananchi kuelewa taratibu zake ili kuepusha changamoto zisizo za lazima.

Naye mkandarasi aliyekabidhiwa utekelezaji wa mradi huo, Bw. Patrick Mong, amesema lengo lao ni kuukamilisha mradi huo ndani ya miezi 33, huku akibainisha kuwa kazi za utekelezaji zinaanza rasmi Februari 9 mwaka huu.Amesema mkandarasi amejiandaa kikamilifu kuhakikisha mradi unakamilika kwa ubora na kwa muda uliopangwa ili wananchi wa Mkoa wa Manyara wanufaike na huduma ya umeme kwa maendeleo endelevu.








No comments:
Post a Comment