Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limetoa elimu ya mazingira kwenye Kongamano la Mwaka la Anwani za Makazi na Maonesho ya Teknolojia ya Huduma za Posta 2026 ihusuyo masuala mazima ya uhufadhi na usimamizi wa mazingira kwa mujibu wa sheria ya mazingira ya mwaka 2004 na kanuni zake katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika kongamano hilo linalotarajiwa kuisha Februari 08, 2026, Mhandisi Mkuu wa NEMC, Bwana Jampyon Mbugi, amesema kuwa matumizi sahihi ya anwani za makazi ni nyenzo muhimu katika kuimarisha usimamizi wa mazingira kupitia mfumo wa NAPA ambao utaiwezesha NEMC kupata taarifa muhimu za yhifadhi na usimamizi wa mazingira.
Ameongeza kuwa elimu hiyo inalenga kuwajengea wananchi uelewa wa majukumu yao ya kisheria na kijamii katika kulinda mazingira. Hata hivyo, anwani za makazi si utambulisho pekee wa maeneo bali ni chombo muhimu cha kupanga makazi na kusimamia mazingira kwa maendeleo yanayozingatia ustawi wa jamii na mazingira kwa ujumla.
Naye Mhandisi Migodi NEMC, Bw. Hezron Mwashibanda ameeleza kuwa huduma zinazotolewa katika banda la NEMC ni pamoja na udhibiti wa kelele chafuzi, ufuatiliaji wa utekelezaji wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM/EIA), pamoja na utekelezaji wa sheria, ada na tozo za mazingira katika maeneo ya makazi na biashara.
NEMC inawakaribisha wananchi na wadau wote wa mazingira kupata elumu ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira.




No comments:
Post a Comment