Na Mwandishi Wetu, Babati – Manyara.
Maafisa Mawasiliano wa Serikali mkoani Manyara wametakiwa kujitathmini, kuimarisha weledi wao na kujipa thamani kazini ili kuongeza ufanisi wa vitengo vya mawasiliano na mchango wake katika utekelezaji wa shughuli za Serikali.
Wito huo umetolewa na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, Bw. Dominic Mbwette, wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha siku mbili cha Maafisa Mawasiliano wa Serikali wa Mkoa wa Manyara kilichofanyika jijini Babati kuanzia Februari 2 hadi 3, 2026.
Bw. Mbwette alisema kuwa changamoto ya kutotambuliwa kwa baadhi ya Vitengo vya Mawasiliano ndani ya taasisi za Serikali inaweza kupatiwa suluhisho endapo Maafisa Mawasiliano wenyewe wataonesha kwa vitendo thamani ya taaluma yao kupitia uwajibikaji, ubunifu na matokeo chanya ya kazi wanazofanya.
“Umuhimu wenu hauamuliwi na cheo pekee bali na matokeo ya kazi zenu. Mkijipa thamani kwa kutekeleza majukumu kwa ufanisi, ni rahisi kwa viongozi na jamii kuona mchango wenu,” alisema Mbwette.
Ameongeza kuwa Maafisa Mawasiliano ni nguzo muhimu ya kuimarisha uwazi, kuwajengea wananchi uelewa wa mipango ya Serikali na kukuza imani kati ya Serikali na jamii, hivyo wanapaswa kutumia fursa hiyo kama sehemu ya kujenga taswira chanya ya utumishi wa umma.
Aidha, aliahidi kuwa Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa itaendelea kutoa miongozo na maelekezo kwa Halmashauri zote ili kuhakikisha Vitengo vya Mawasiliano vinapatiwa rasilimali na bajeti stahiki kwa utekelezaji wa majukumu yao.
Kwa upande wao, Maafisa Mawasiliano walieleza kuwa kikao kazi hicho kimewapa fursa ya kubadilishana uzoefu, kuimarisha ujuzi na kuweka mikakati ya pamoja ya kuboresha utoaji wa taarifa za Serikali kwa wananchi.
Bw. Mbwette alihitimisha kwa kuwataka Maafisa Mawasiliano kuendelea kufanya kazi kwa weledi, uzalendo na nidhamu ili kuimarisha uwajibikaji na uwazi katika utumishi wa umma mkoani Manyara.









No comments:
Post a Comment