HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, February 13, 2026

ITHIBATI YA UMAHIRI KATIKA UKAGUZI WA MIFUMO KULETA TIJA SOKO LA KIMATAIFA

Kupatikana kwa ithibati ya umahiri wa kimataifa katika mfumo wa ukaguzi wa ISO/IEC 17020 ni hatua kubwa itakayoiondolea Tanzania vikwazo vya kiufundi katika biashara. 

Aidha, ni uthibitisho wa weledi na uadilifu wa Serikali katika kudhibiti ubora, hatua inayoongeza imani ya wadau wa ndani na nje ya nchi kwa bidhaa zinazozalishwa nchini.

Hayo yamesemwa Februari 13, 2026, na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Salvio Kapinga (Mb.), katika hafla ya kihistoria ya kukabidhiwa cheti cha ithibati ya umahiri wa mfumo wa ukaguzi kwa kiwango cha kimataifa (ISO/IEC 17020). Cheti hicho kimetolewa na Taasisi ya SADCAS kwenda kwa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Waziri Kapinga amesisitiza kuwa umuhimu wa ithibati hiyo unadhihirisha uwezo wa Tanzania kushindana kwenye masoko ya kikanda na kimataifa bila kutiliwa shaka. Mfumo huo wa ISO unahakikisha kuwa shughuli za ukaguzi zinazofanywa na TBS zinakidhi vigezo vya kimataifa, hivyo kurahisisha upatikanaji wa masoko, kuimarisha usalama wa bidhaa kwa ajili ya kulinda afya za walaji, na kukuza uchumi wa Taifa kwa ujumla.

Aidha, Waziri Kapinga amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uongozi wake thabiti uliowezesha kuwepo kwa mazingira bora ya biashara na uwekezaji. 

Uongozi huo umeimarisha miundombinu ya TBS na mifumo ya udhibiti ili kuhakikisha bidhaa za Kitanzania zinapata thamani stahiki kuelekea mapinduzi ya viwanda na kuimarisha ushindani wa kibiashara.

Vilevile, Waziri ameishukuru Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (EU) na Shirika la Maendeleo ya Viwanda la Umoja wa Mataifa (UNIDO) kwa ushirikiano wao wa kimkakati huku akiipongeza TBS kwa kupata cheti hicho na kutoa wito kwa watumishi wa TBS na wadau wa sekta binafsi kuilinda ithibati hiyo kwa "wivu mkubwa", uadilifu wa hali ya juu, na uendelevu wa mifumo ya kiutendaji. 

Hatua hiyo italenga kuvutia uwekezaji na kuhakikisha kuwa Tanzania inabaki kuwa kitovu cha bidhaa bora katika ukanda wa SADC na duniani kote.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Ashura Katunzi, amebainisha kuwa mafanikio hayo ni matunda ya dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kulinda afya ya walaji na kukuza uchumi.

Amebainisha kuwa TBS imekuwa taasisi ya kwanza nchini na ya pili katika ukanda wa Afrika Mashariki kupata ithibati hiyo kutoka SADCAS, ikithibitisha kuwa mifumo ya ukaguzi ya shirika hilo inakidhi vigezo vya kimataifa katika maeneo ya uzalishaji, bandarini na mipakani.

Dkt. Katunzi amefafanua kuwa mchakato huo uliodumu kwa zaidi ya mwaka mmoja ulihusisha tathmini za kina zilizokamilika mnamo Oktoba 2025. 

Alihitimisha kwa kutoa ahadi kuwa TBS itaendelea kuboresha utendaji wake kwa weledi na uadilifu ili kuhakikisha huduma zinazotolewa zinabaki kuwa shindani na zenye viwango vya juu duniani.


















No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad