HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, February 25, 2026

GF TRUCKS YAWASHIKA MKONO FEMATA SAFARI YA CANADA

 


Kampuni ya GF Trucks & Equipment’s Ltd imeungana na Chama cha Wachimbaji Madini Wadogo Tanzania (FEMATA) katika safari ya kwenda nchini Canada kushiriki maonesho ya teknolojia ya madini.

GF, ambao ni wadau na walezi wa wachimbaji hao, wametoa pongezi na mkono wa baraka kufuatia mwaliko huo wa kushiriki maonyesho makubwa ya kimataifa. Ushiriki huo unatarajiwa kufungua fursa ya kujifunza teknolojia za kisasa zitakazosaidia kuongeza thamani ya madini ya Tanzania, hususan madini ya lithium na cobalt yanayotumika kutengeneza betri za magari ya umeme.

Kupitia mafunzo na uzoefu watakaoupata, wachimbaji hao wanatarajia kuchangia upatikanaji wa malighafi za uhakika kwa viwanda vya ndani, ikiwemo sekta ya uunganishaji wa magari, jambo litakalosaidia kukuza uchumi wa nchi na kuongeza ajira.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa hafla ya kuwaaga washiriki wa safari hiyo, Katibu Mkuu wa FEMATA, Rogers Micheal Sezero, aliishukuru GF kwa kuendelea kuwashika mkono wachimbaji wadogo. Alisema ushirikiano huo umechangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa wachimbaji siku hadi siku.

Alieleza kuwa GF imekuwa na mpango maalum wa kuwakopesha wachimbaji wadogo vitendea kazi badala ya fedha taslimu, hatua iliyowezesha wengi wao kumiliki mitambo na magari ya kazi kwa urahisi zaidi. Mpango huo rafiki umesaidia kuongeza tija na ufanisi katika shughuli zao za uchimbaji.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa safari hiyo na mmoja wa wachimbaji, Dkt. Bernard Joseph, alisema licha ya kuwepo kwa makampuni mengi yanayofanya biashara na wachimbaji, GF imekuwa mstari wa mbele kuwasaidia wanapohitaji msaada.

“Tunapoenda kuitangaza FEMATA nchini Canada, GF wametupatia mahitaji muhimu ya safari na hawajawahi kutuacha tunapowahitaji kwa jambo dogo au kubwa. Kupitia programu zao za mafunzo kwa wachimbaji na madereva, nami ni mmoja wa wanufaika. Safari hii itanisaidia kuongeza ujuzi zaidi,” alisema Dkt. Joseph.

Naye Mkurugenzi wa Masoko na Mawasiliano wa GF, Salman Karmali, alisema katika kuadhimisha miaka 19 ya kampuni hiyo, wameona ni vyema kurejesha kwa jamii kwa kuwawezesha FEMATA kushiriki maonyesho hayo ya teknolojia ya madini nchini Canada.

Aliongeza kuwa kabla ya safari hiyo, GF imekuwa ikiendesha semina na mafunzo katika maeneo mbalimbali yenye shughuli za madini kama Geita, Mwanza, Songwe na Lindi. Kupitia semina hizo, zaidi ya madereva na waendesha mitambo 1,000 kutoka makampuni tofauti wamepatiwa mafunzo ya matumizi ya teknolojia za kisasa, hasa ikizingatiwa kuwa magari na mitambo ya sasa yanatumia teknolojia inayobadilika kwa kasi.

GF ni wauzaji wa magari ya mizigo ya FAW na mitambo ya XCMG, na wanajivunia kuadhimisha miaka 19 tangu kuanzishwa kwake. Kampuni hiyo pia inamiliki kiwanda cha kuunganisha magari kilichopo Kibaha, mkoani Pwani, ikiwa ni miongoni mwa viwanda vya kwanza vya aina hiyo nchini.
Mkuu wa kitengo cha mauzo wa kampuni ya GF Trucks & Equipment's  kanda ya ziwa, Poul Msuku akizungumza na viongozi wa chama cha wachimbaji wadogo (FEMATA)  wakati wa hafla ya kuwaaga kwa ajili ya safari ya wachimbaji wadogo nchini Canada kushiriki  maonesho na mafunzo ya teknolojia ya madini jijini Dar es salaam.Kulia ni Mkurugenzi wa asoko na mawasiliano wa  GF ,Salman Karmal
Mwenyekiti wa Safari ya wachimbaji wadogo nchini Canada ,Benard Joseph akizungumza na waandishi wa habari wakati wa hafla ya kuwaaga na kukabidhiwa vifaa na kampuni ya GF iliyofanyika jijini Dar es salaam
Mkurugeni wa masoko na mwasiliano wa kampuni ya GF,Salman Karmali(wa pili kushoto) akiwa na viongozi wa chama cha wachimbaji wadogo akiwakabidhi vitendendea kazi wakati wa hafla ya kuwaaga kabla ya kuanza safari ya nchini Canada kushiriki maonesho ya Madini hafla iliyofanyioka jijini Dar es salaam

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad