HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, February 25, 2026

Geita Kuimarisha Mapambano Dhidi ya VVU Miongoni mwa Wachimbaji Wadogo

 

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita Dkt. Omary Sukari (aliesimama) akiongoza majadiliano wakati wa kikao kazi kilichokutana jijini Mwanza kupanga mikakati itakayotumika kufikisha huduma za VVU na UKIMWI kwa wachimbaji wadogo mkoani Geita.

Na Mwandishi Wetu
WADAU mbalimbali wamekutana jijini Mwanza katika kikao kazi maalum chenye lengo la kuimarisha mwitikio wa VVU miongoni mwa wachimbaji wadogo mkoani Geita, hatua inayolenga kuongeza kasi ya kufikia malengo ya kitaifa na kimataifa ya kudhibiti maambukizi ya Virusi vya UKIMWI.

Kikao hicho kimefanyika katika kipindi muhimu, ikizingatiwa kuwa Mkoa wa Geita unakadiriwa kuwa na takriban asilimia 10 ya jumla ya wachimbaji wadogo milioni nne waliopo nchini Tanzania, wanaofanya kazi katika zaidi ya maeneo 100 ya uchimbaji. Licha ya kiwango cha maambukizi ya VVU mkoani Geita kwa ujumla kuwa asilimia 4.9, tafiti zinaonesha kuwa katika jamii za wachimbaji wadogo kiwango hicho kinakisiwa kufikia asilimia 9.3, karibu mara mbili ya wastani wa mkoa.

Aidha, mkoa huo kwa sasa umefikia kati ya asilimia 60 hadi 70 tu ya lengo la kwanza la 95 chini ya mfumo wa kimataifa wa 95–95–95, unaolenga kuhakikisha asilimia 95 ya watu wanaoishi na VVU wanajua hali zao, asilimia 95 ya wanaojua hali zao wanaanza matibabu, na asilimia 95 ya wanaopata matibabu wanafikia udhibiti wa virusi. Hii ina maana kuwa bado kuna idadi kubwa ya watu wanaoishi na VVU ambao hawajui hali zao.

Kikao hicho kiliwakutanisha wawakilishi kutoka Geita Gold Mining Limited (GGML), GGML Kilimanjaro Challenge Against HIV/AIDS Trust, Tanzania Commission for AIDS (TACAIDS), mamlaka za Serikali ya Mkoa na Serikali za Mitaa, waratibu wa VVU na UKIMWI pamoja na washirika wengine wa maendeleo. Lengo kuu lilikuwa kubuni afua mahsusi zenye matokeo makubwa na zinazolingana na mazingira halisi ya wachimbaji wadogo wa Geita.

Kupitia Kili Grants Portfolio ya mwaka 2024/2025, Trust imetenga shilingi milioni 100 kusaidia utekelezaji wa afua zitakazotekelezwa kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia Machi 1, 2026.

Washiriki walibaini changamoto kadhaa zinazoathiri mwitikio wa VVU katika jamii za wachimbaji, ikiwemo uelewa mdogo kuhusu kinga, upimaji na matibabu; ushiriki mdogo katika huduma za upimaji; uhamaji mkubwa wa wachimbaji unaoathiri ufuatiliaji na mwendelezo wa matibabu; pamoja na unyanyapaa, imani potofu na uwepo wa jumbe zisizo thabiti katika maeneo ya uchimbaji.

Akizungumza katika kikao hicho, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita, Dkt. Omar Sukari, alisema hatua ya kwanza itakuwa kutoa elimu ya kina kwa jamii, hasa wale wanaofanya kazi katika migodi midogo inayozunguka mgodi wa GGM, ili kuwapatia maarifa sahihi kuhusu VVU na kuwahamasisha kujitokeza kupima.

Kwa mujibu wa mpango huo, huduma za upimaji wa VVU kupitia vituo vinavyohama zitaifikia moja kwa moja jamii za wachimbaji katika maeneo yao ya kazi. Lengo ni kuwafikia zaidi ya wachimbaji wadogo 5,000 na kuhakikisha wanaopatikana na maambukizi wanaunganishwa haraka katika Kliniki za Huduma na Matibabu (CTC) kwa ajili ya kuanza tiba.

Mratibu wa VVU na UKIMWI Mkoa wa Geita, Dkt. Yohane Kiaga, alisema mkoa unaliona zoezi hilo kuwa fursa muhimu kwa kuwa fedha zinazotumika zinatokana na juhudi za Watanzania wenyewe kupitia Kili Challenge. Aliongeza kuwa pamoja na kuwafikia wachimbaji, mpango huo pia utahusisha takriban shule 15 zilizopo katika maeneo ya uchimbaji ili kuimarisha elimu ya kinga kwa vijana balehe.

Mbali na huduma za upimaji, mpango huo utatumia vifaa vya mawasiliano ya mabadiliko ya tabia (IEC) vyenye ubunifu na vinavyodumu, ikiwemo michoro ya ukutani, mabango na vipeperushi vitakavyowekwa katika maeneo ya uchimbaji kama vikumbusho vya kudumu hata baada ya shughuli za uhamasishaji kukamilika.

Katika kipindi cha utekelezaji, wadau watabaini na kuchora ramani ya maeneo muhimu ya uchimbaji, kuratibu na mamlaka za mitaa pamoja na vituo vya afya, kufanya kampeni za uhamasishaji na upimaji, na kufuatilia idadi ya watu waliopimwa pamoja na wale waliounganishwa kwenye huduma za matibabu. Mafanikio ya mpango yatapimwa kwa kuangalia idadi ya waliopatikana, waliopimwa na waliounganishwa kwenye tiba.

Matokeo yanayotarajiwa ni kuongezeka kwa uelewa wa VVU miongoni mwa wachimbaji wadogo, zaidi ya watu 5,000 kupimwa, kuimarika kwa kasi ya kufikia lengo la kwanza la 95, kupungua kwa unyanyapaa katika jamii za uchimbaji na kuimarika kwa uratibu wa wadau mbalimbali.

Mpango huu unaakisi dhamira endelevu ya GGML Kilimanjaro Challenge Against HIV/AIDS Trust ya kupunguza athari za VVU na UKIMWI nchini Tanzania kwa kuwekeza rasilimali moja kwa moja katika jamii zilizo hatarini zaidi. Utekelezaji utakapoanza Machi 1, 2026, mshikamano uliooneshwa na wadau unatarajiwa kuweka msingi imara wa kuharakisha mafanikio katika mapambano dhidi ya VVU miongoni mwa wachimbaji wadogo wa Mkoa wa Geita.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad