ALN Tanzania, kampuni inayojishughulisha katika huduma za kisheria na ushauri wa biashara, imezitaka biashara za kifamilia nchini kuondokana na mifumo isiyo rasmi iliyowasaidia katika hatua za awali za ukuaji, na badala yake kukumbatia mifumo thabiti ya utawala bora.
Hatua hiyo itawezesha kulinda utajiri wa vizazi, kuhakikisha ustawi wa muda mrefu na kuvutia uwekezaji kutoka nje.
Wito huo ulitolewa wakati wa hitimisho la mfululizo wa semina za mafundisho ya kusimamia biashara za kifamilia katika mfumo sahihi ( Family Business Resilience & Growth Knowledge Series), zilizoandaliwa na ALN Tanzania kwa ushirikiano na International Finance Corporation (IFC) jijini Dar es Salaam wiki hii. Mfululizo huo semina hizo tatu ulijadili misingi ya utawala wa kifamilia, muundo wa bodi na katiba za familia katika awamu zilizopita, huku kikao cha mwisho kikijikita katika urithishaji na mpito wa uongozi.
Akizungumza katika semina hiyo, Shemane Amin, Mshirika wa ALN hapa nchini , alisisitiza kuwa mwendelezo wa biashara za kifamilia hauji kwa mazoea bali unapaswa kupangwa kwa makusudi.
“Biashara nyingi za kifamilia hukua kwa mafanikio katika miaka ya mwanzo kwa kutegemea imani na maamuzi yasiyo rasmi,” alisema. “Hata hivyo, kadri biashara zinavyopanuka na vizazi vinavyoongezeka kushiriki, kuweka mifumo rasmi kunakuwa muhimu kulinda biashara yenyewe na umoja wa familia.”
Alieleza kuwa kampuni hiyo ilianzisha mfululizo huo wa semina ili kuwapatia wamiliki wa biashara za kifamilia mifumo ya vitendo kuhusu utawala bora, upangaji wa urithishaji na uwazi wa uongozi mambo ambayo mara nyingi huamua iwapo biashara itaendelea baada ya kizazi cha mwanzilishi wa biashara (Founder) katika familia husika.
Kwa upande wake, Edward Williams, Mkurugenzi wa ALN Tanzania, alisisitiza umuhimu wa kuanza mapema kupanga urithishaji na kuonya dhidi ya mabadiliko ya uongozi yanayofanyika kwa dharura.
“Moja ya dhana potofu iliyoenea katika biashara za kifamilia ni kwamba urithishaji huanza pale mwanzilishi anapokuwa tayari kustaafu,” alisema. “Kwa uhalisia, urithishaji huanza mapema zaidi.
Mabadiliko yenye mafanikio ni yale ambayo ukuzaji wa uongozi, miundo ya wanahisa na mifumo ya utawala inakuwa tayari imewekwa tangu awali.”, alisema.
Alibainisha kuwa kadri biashara za Kitanzania zinavyokua kwa thamani na kuwa tata zaidi, mikataba rasmi ya wanahisa, katiba za familia, majukumu yaliyoainishwa wazi kwa watendaji wakuu na mifumo huru ya usimamizi vinakuwa muhimu katika kulinda thamani ya muda mrefu.
Naye Mona Doshi, Mshirika wa ALN kutoka Mombasa nchini Kenya, alizungumzia umuhimu wa sera rasmi za ajira kwa wanafamilia katika kuimarisha uimara wa biashara.
“Kadri familia zinavyopanuka kizazi hadi kizazi, kuwa na mwongozo wa uwazi kuhusu vigezo vya kuajiriwa, viwango vya utendaji na uwajibikaji husaidia kuzuia migogoro ya ndani na kuimarisha uongozi unaozingatia sifa,” alieleza.
Aliwahimiza wamiliki wa biashara kuweka mifumo rasmi ya utawala inayolinda urithi wa familia huku ikizingatia weledi, ili kuhakikisha mabadiliko ya uongozi yanategemea maandalizi na uwezo wa mtu badala ya kuchaguliwa kuongoza tu kwa sababu ni sehemu ya familia.
Akizungumza kwa niaba ya IFC, Rose Lumumba alisisitiza kuwa utawala bora uliowekwa kwa mifumo rasmi unahusishwa moja kwa moja na utayari wa kupokea uwekezaji na ustawi wa muda mrefu.
“Biashara za kifamilia zinazoweka mifumo ya utawala mapema huwa katika nafasi nzuri zaidi ya kuvutia mitaji, kupanuka kwa uwajibikaji na kustahimili mabadiliko ya vizazi,” alisema.
Washiriki walikubaliana kuwa biashara za kifamilia zina mchango mkubwa katika uchumi wa Tanzania, na kwamba uwezo wake wa kuweka mifumo rasmi ya uongozi na utawala utaathiri uimara wa sekta binafsi kwa ujumla.
Tafiti za kimataifa zinaonesha kuwa ingawa biashara za kifamilia zinachangia zaidi ya asilimia 60 ya shughuli za sekta binafsi duniani, ni takriban asilimia 30 tu zinazofanikiwa kuvuka hadi kizazi cha pili, na chini ya asilimia 15 hufikia kizazi cha tatu. Wataalamu wa sekta hiyo wanaeleza kuwa upangaji madhubuti wa urithishaji na nidhamu ya utawala bora huongeza kwa kiasi kikubwa uwezekano wa mafanikio ya mpito huo.
ALN Tanzania hutoa ushauri kwa biashara za kifamilia kuhusu uundaji wa mifumo ya utawala, mipango ya urithishaji, makubaliano ya wanahisa na suluhisho za usimamizi wa utajiri wa kuvuka mipaka, ikiwawezesha kubadilika kutoka biashara zinazoongozwa na waanzilishi hadi taasisi imara za kudumu.
Bi. Shemane Amin, Mshirika wa ALN Tanzania (kulia), akiendesha mazungumzo na Bw. Vineet Verma, Meneja Mkuu wa Kioo Limited, wakati wa hitimisho la mfululizo wa Uendeshaji kimfumo wa biashara za kifamilia ( Family Business Resilience & Growth Knowledge Series), ulioandaliwa kwa ushirikiano kati ya ALN na International Finance Corporation (IFC) jijini Dar es Salaam wiki hii.

Bw. Edward Williams, Mkurugenzi wa ALN Tanzania, akiongea wakati wa hitimisho la mfululizo wa kongamano la mafunzo ya uendeshaji kimfumo wa biashara za kifamilia (Family Business Resilience & Growth Knowledge Series), ulioandaliwa kwa ushirikiano kati ya ALN na International Finance Corporation (IFC) jijini Dar es Salaam wiki hii.
Baadhi ya washiriki wa hitimisho la mfululizo wa kongamano la mafunzo ya uendeshaji bora wa biashara za kifamilia ( Family Business Resilience & Growth Knowledge Series), ulioandaliwa na ALN Tanzania kwa ushirikiano na International Finance Corporation (IFC) jijini Dar es Salaam wiki hii.



No comments:
Post a Comment