

Zanzibar, 10 Februari 2026.
KAMPUNI ya mawasiliano ya simu ya Airtel Tanzania leo inazindua rasmi maduka manne mapya ya kisasa katika Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar. Hafla ya uzinduzi imefanyikia katika eneo la ZSSF Mbweni na imerasmishwa na Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Bw. Mohamed Abdallah.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Bw. Mohamed Abdallah, amepongeza uwekezaji wa Airtel na kusema kuwa upanuzi wa huduma za mawasiliano ni kichocheo muhimu cha maendeleo ya kiuchumi na kijamii Zanzibar.
“Huduma bora za mawasiliano na fedha kidijitali zinaimarisha biashara, zinawaunganisha wananchi na fursa mpya, na kusaidia kukuza sekta muhimu kama utalii na uchumi wa bluu. Tunakaribisha uwekezaji huu unaoleta huduma karibu zaidi na wananchi wetu,” anasema Bw. Abdallah.
Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa Airtel Tanzania, Bi. Adriana Lyamba, anasema kuwa hatua hii ni sehemu ya mkakati mkubwa wa kampuni wa kuhakikisha huduma zake zinawafikia wateja kwa urahisi zaidi huku ikiendelea kuboresha uzoefu wao kila siku.
“Maduka haya ni vituo vya kisasa vinavyowawezesha wateja kupata huduma zote za mawasiliano pamoja na huduma za fedha kidijitali kwa urahisi na haraka, mahali pamoja,” anasema Bi. Lyamba.
Anaongeza kuwa uwekezaji huu unafungua milango ya fursa za kiuchumi, ambapo kila duka linanufaisha zaidi ya wajasiriamali na wafanyabiashara 400 wanaotegemea mawasiliano na malipo ya kidijitali katika kuendesha shughuli zao za kila siku. Hivyo, maduka haya si tu yanaboresha upatikanaji wa huduma, bali pia yanachochea ukuaji wa biashara na ajira katika jamii.
Bi. Lyamba anasisitiza umuhimu wa Zanzibar kama kitovu cha utalii na sehemu muhimu ya uchumi wa bluu unaokua kwa kasi. Anaeleza kuwa Airtel inaendelea kuwekeza katika huduma za fedha kidijitali na intaneti yenye kasi ili kusaidia sekta za utalii, shughuli za baharini na huduma nyingine zinazochangia maendeleo ya kiuchumi ya visiwa hivyo.
“Dhamira yetu ni kuhakikisha wakazi wa Zanzibar, wafanyabiashara na wageni wanaotembelea visiwa hivi wanapata mawasiliano ya uhakika na huduma za kifedha zilizo salama na rahisi kutumia. Hii ni sehemu ya ahadi yetu ya kuhakikisha kuwa Airtel inawafikia watu kila kona, tukileta teknolojia karibu na maisha yao ya kila siku,” anaongeza.


.jpeg)
No comments:
Post a Comment