HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, January 10, 2026

Waziri wa Kilimo Chongolo aridhishwa na maendeleo ya ushirika, atoa hamasa ya kuongeza kasi zaidi

Na Mwandishi wetu

Dar es Salaam. Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, amesema ameridhishwa na maendeleo makubwa yaliyopatikana katika sekta ya ushirika nchini, akisisitiza kuwa mafanikio hayo ni kielelezo cha imani kubwa ambayo Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.

Pia amesema pamoja na hatua zilizofikiwa, bado kuna wajibu mkubwa kwa wanaushirika na wadau wote kuongeza juhudi ili sekta hiyo iendelee kuwa kichocheo cha maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla.

Waziri Chongolo amesema hayo wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 30 wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania (TFC) uliofanyika katika Ukumbi wa Johari Rotana Hotel, akihudhuriwa na viongozi wa vyama vya ushirika kutoka mikoa mbalimbali nchini pamoja na wadau wa sekta hiyo.

Amesema mkutano huo ni tukio muhimu linaloashiria umoja, mshikamano na dira ya pamoja ya wanaushirika, sambamba na kuwa jukwaa la kufanya maamuzi yenye manufaa ya muda mfupi, wa kati na mrefu.

Waziri Chongolo alisema Serikali inaendelea kuwa na imani kubwa na sekta ya ushirika kutokana na mchango wake unaoonekana katika nyanja mbalimbali ikiwemo kuongeza uzalishaji, kuboresha maisha ya wakulima na wanachama, pamoja na kuchochea uchumi wa taifa.

Alisisitiza kuwa imani hiyo ni dhamana kwa wanaushirika kuhakikisha wanafanya kazi kwa bidii, uwazi na weledi ili kuleta tija zaidi.

Waziri Chongolo pia aliwapongeza wanaushirika kwa mafanikio yaliyopatikana, akitaja miongoni mwao ni uanzishwaji wa Benki ya Ushirika Tanzania inayomilikiwa kwa asilimia 51 na wanaushirika.

Alisema kuwa hatua hiyo ni ya kihistoria na kimkakati katika kutatua changamoto za muda mrefu za mitaji na huduma za kifedha.

Aliongeza pia ujenzi na ufufuaji wa viwanda vya kuongeza thamani ya mazao, ujenzi wa maghala ya kuhifadhi mazao, kuwaunganisha wanaushirika na masoko ya uhakika, pamoja na kurahisisha utekelezaji wa sera za serikali ikiwemo usambazaji wa mbolea, mbegu na pembejeo za ruzuku.

“Sekta ya ushirika imekuwa chombo muhimu katika kuwezesha upatikanaji wa mikopo kupitia SACCOS, kuandaa Mpango Kabambe wa Sekta ya Ushirika (Cooperative Development Master Plan), na kuongeza ajira rasmi na zisizo rasmi nchini,”alisema Waziri Chongolo.

Hata hivyo, Waziri alisisitiza kuwa mafanikio hayo yasiwe sababu ya kuridhika, bali yawe chachu ya kuongeza kasi katika maeneo muhimu kama ushiriki wa vyama vya ushirika kwenye uchumi wa viwanda, matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama), bima za mazao, nishati safi na utunzaji wa mazingira.

Waziri Chongolo pia alisisitiza umuhimu wa vyama vya ushirika kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Dira ya Wizara ya Kilimo na Mpango Kabambe wa Sekta ya Ushirika, sambamba na kubuni huduma na bidhaa zitakazowavutia vijana kujiunga na ushirika.

Aidha, alihimiza kuimarishwa kwa mtaji wa Benki ya Ushirika, uwekezaji wenye tija, ajira za watumishi wenye sifa, na kuwepo kwa mipango ya ruzuku kwa wanachama ili kuongeza uzalishaji na kuvutia wanachama wapya.

Kwa upande wa utawala bora, Waziri Chongolo alitoa onyo kali dhidi ya ubadhirifu na ufujaji wa mali za ushirika, akisema Serikali haitasita kuchukua hatua za kisheria kwa viongozi wasiowaadilifu.

Alisisitiza kuwa uadilifu, uwajibikaji na uaminifu ni nguzo muhimu za kujenga taswira chanya ya sekta ya ushirika na kuimarisha imani ya wanachama.

Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa TFC, Tito Haule, aliipongeza Serikali ya Rais Samia kwa mchango mkubwa uliowezesha sekta ya ushirika kupiga hatua.

Alisema TFC imeanza mageuzi makubwa ikiwemo kufanya uhakiki wa mahesabu na kwa mara ya kwanza baada ya miaka 10 kupata hati safi ya ukaguzi.

Aliongeza kuwa TFC imeanzisha jukwaa la Coop Talk kwa ajili ya kubadilishana taarifa na changamoto, pamoja na kuongeza wanachama na wigo wa shirikisho.

Naye Mtendaji Mkuu wa TFC, Fares Muganda, alisema juhudi zinaendelea kupanua wigo wa sekta kwa kushirikiana na wadau, huku zoezi la bima kwa wanachama likianza kwa majaribio katika wilaya tatu za mkoa wa Tabora.

Kwa upande wake, Mrajis wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania, Dkt. Benson Ndiege, alihimiza TFC kuwaunganisha wakulima na masoko ya kitaifa na kimataifa, kurahisisha mikopo, kudhibiti ulanguzi wa bei na kusimamia usajili wa wanachama katika mifumo ya kidigitali ili kuboresha utoaji wa huduma.
Waziri wa Kilimo Daniel Chongolo akizungumza wakati wa Mkutano Mkuu wa 30 wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania (TFC) uliofanyika katika Ukumbi wa Johari Rotana Hotel jijini  Dar es Salaam.
Waziri wa Kilimo Daniel Chongolo (Kulia) akipokea cheti kutoka kwa Mrajis wa Vyama Vya Ushirika Tanzania Dkt Benson Ndiege mara baada ya kuzindua jukwaa maalum la ushirika lijulikanalo kwa Coop Talk.
Waziri wa Kilimo Daniel Chongolo (kushoto) akizindua jukwaa maalum la kupata taarifa mbalimbali za masuala ya ushirikia lijulikanalo kwa jina la Coop Talk wakati wa Mkutano Mkuu wa 30 wa sekta hiyo ulifanyika kwenye hotel ya Johari Rotana.
Mtendaji Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania (TFC), Fares Muganda akisisitiza jambo wakati wa Mkutano Mkuu wa 30 wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania (TFC) uliofanyika katika Ukumbi wa Johari Rotana Hotel jijini  Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Ushirika Tanzania, Tito Haule akihutubia wakati wa Mkutano Mkuu wa 30 wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania (TFC) uliofanyika katika Ukumbi wa Johari Rotana Hotel jijini  Dar es Salaam.
Mrajis wa Vyama vya Ushirika Tanzania, Dkt Benson Ndiege, akizungumza wakati wa Mkutano Mkuu wa 30 wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania (TFC) uliofanyika katika Ukumbi wa Johari Rotana Hotel jijini Dar es Salaam.
Washiriki mbalimbali wakifuatilia wa Mkutano Mkuu wa 30 wa sekta hiyo ulifanyika kwenye hotel ya Johari Rotana.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad