Watendaji wa uchaguzi wametakiwa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na weledi ili kufanikisha uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Peramiho na udiwani katika Kata ya Shiwinga unaotarajiwa kufanyika tarehe 26 Februari, 2026.
Wito huo umetolewa na Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufaa (Mst) Mbarouk Salim Mbarouk Mkoani Iringa leo tarehe 26 Januari, 2026 wakati akifunga mafunzo ya watendaji wa uchaguzi yaliyofanyika kwa siku tatu kuanzia tarehe 24 Januari, 2026.
“Ni matazamio ya Tume kwamba, baada ya kupatiwa mafunzo haya, mtatekeleza majukumu yenu kwa ufanisi na weledi mkizingatia ratiba ya utekelezaji ili kufanikisha uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Peramiho na Udiwani katika Kata ya Shiwinga unaotarajiwa kufanyika tarehe 26 Februari, 2026,” amesema Jaji Mbarouk.
Amesisitiza kuwa ili ufanisi uwepo ni muhimu watendaji hao wazingatie sifa na uwezo wakati wa kuteua na kuajiri watendaji wa vituo vya kupigia kura kwa kuwa hao ndio watakaosimamia zoezi la kupiga kura na kuhesabu kura vituoni.
“Kuhusu ajira za kupata watendaji wa vituo, tunayo imani kuwa mtateua na kuajiri watendaji wenye sifa na uwezo wa kufanya kazi hii muhimu……kwa kuwa hao ndio watakaosimamia zoezi la kupiga kura na kuhesabu kura vituoni. Kazi ambayo inahitaji umahiri, umakini na weledi katika kuitekeleza,” amesema Jaji Mbarouk.
Amewataka watendaji hao kuhakikisha kuwa mafunzo ya watendaji wa vituo yanafanyika kwa ufanisi na weledi katika tarehe zilizopangwa kwenye ratiba ya utekelezaji wa shughuli za uchaguzi.
Ameongeza kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo ili waweze kufahamu majukumu yao na kuyatekeleza ipasavyo wakati wa uchaguzi.
Jaji Mbarouk amewakumbusha watendaji hao kuwa shughuli zote za uchaguzi zinaongozwa na Katiba, sheria, kanuni, maadili ya uchaguzi na maelekezo ya Tume na kuongeza kuwa kuna umuhimu wa kutenga sehemu ya muda wao kusoma Katiba, sheria na maelekezo mbalimbali yanayotolewa na Tume ili yawaongoze katika kusimamia uchaguzi utakaokuwa huru na wa haki.
Mafunzo hayo yamewahusisha Waratibu wa Uchaguzi wa Mikoa ya Songwe na Ruvuma, Wasimamizi wa Uchaguzi, Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi Ngazi ya Jimbo, Wasimamizi wa Uchaguzi Ngazi ya Kata, Maafisa Uchaguzi, Maafisa Ununuzi na Wahasibu.
Mada kadhaa ziliwasilishwa ikiwa ni pamoja na Majukumu ya Watendaji wa Uchaguzi, Mambo Muhimu ya Kuzingatia, Uteuzi wa Wagombea, Maadili na Kampeni za Uchaguzi, Wajibu na Majukumu ya Watendaji wa Vituo na Utambulisho wa Mawakala wa Vyama vya Siasa, Taratibu za Upigaji Kura, Taratibu za Kuhesabu Kura, Kujumlisha Kura na Kutangaza Matokeo, Fomu Zinatotumika kwenye Uchaguzi, Mapokezi na Utunzaji wa Vifaa vya Uchaguzi na Usimamizi wa Fedha za Uchaguzi.


No comments:
Post a Comment