HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, January 31, 2026

WALIMU NA WANAFUNZI WA SHULE YA MSINGI MASHUJAA WATEMBELEA MAKTABA YA MKOA RUVUMA



TIMU ya walimu watatu kutoka Shule ya Msingi Mashujaa ilitembelea Maktaba ya Mkoa Ruvuma kwa lengo la kujifunza na kupata uelewa wa kina kuhusu huduma mbalimbali zitolewazo na maktaba hiyo, pamoja na kujifunza masuala tofauti yanayohusiana na matumizi ya maktaba katika kukuza taaluma.

Ujio wa walimu hao ambao wametembelea Januari 30, 2026,umeonesha matokeo chanya zaidi kwa wanafunzi wa Darasa la Saba waliokuwa pamoja nao, ambapo walionesha umakini mkubwa katika kufanya udadisi wa vitabu wanavyovitumia shuleni. Wanafunzi hao wameeleza kufurahishwa sana na uwepo wa Maktaba ya Mkoa Ruvuma, wakibainisha kuwa maktaba hiyo itakuwa sehemu muhimu ya kuongeza ufaulu wao katika mitihani ya Darasa la Saba watakayoifanya mwishoni mwa mwaka huu.

Kwa upande wao, walimu wamevutiwa na vitengo mbalimbali vilivyopo ndani ya maktaba, vikiwemo kitengo cha watoto, kitengo cha wasomaji watu wazima, kitengo cha wanafunzi wa sekondari, pamoja na vitabu vya mitaala vilivyopo katika kitengo cha TEHAMA ambavyo vinapatikana katika mfumo wa softcopy. Walimu hao wameeleza kuwa huduma hizo zitakuwa msaada mkubwa katika kuboresha mbinu za ufundishaji na ujifunzaji shuleni.

Kwa ujumla, ziara hiyo imezidi kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za elimu, hususan shule na maktaba, katika juhudi za pamoja za kukuza utamaduni wa kusoma na kuongeza ubora wa elimu kwa wanafunzi.

Pichani ni Mkutubi wa Mkoa, ndg. Emmanuel Mwita, watumishi wa maktaba ya mkoa Ruvuma pamoja na walimu walioambatana na wanafunzi hao wa darasa la Saba. Shule ya msingi Mashujaa.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad