MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imejipanga kuanzisha bonanza la michezo litakalofanyika kila robo mwaka kwa watumishi wake nchi nzima, ikiwa ni mkakati wa kuimarisha afya ya mwili na akili pamoja na kuongeza ari na mshikamano kazini.
Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, amesema leo Januari 25, 2026, katika viwanja vya Gymkhana, Dar es Salaam, wakati wa bonanza la michezo litakalotumika pia kama jukwaa la kuhamasisha ulipaji kodi na kulinda jamii.
Amesema bonanza hilo linalenga kuwashirikisha watumishi wote wa TRA ili kujenga umoja, afya njema na ari ya kazi, huku akibainisha kuwa litakuwa likifanyika kila robo mwaka katika vituo vyao nchini.
“Hii natamani ifanyike kwa watumishi wote wa TRA. Nadhani tuanze kufanya bonanza kila robo mwaka kwa nchi nzima, tukiwa na maudhui ya kuhamasisha walipaji kodi na kulinda jamii,” alisema Mwenda.
Kamishna Mwenda ameongeza kuwa bonanza hilo limefanyika ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Forodha Duniani, ambayo kilele chake ni leo, ikiwa ni sehemu ya kuthamini kazi kubwa inayofanywa na mawakala wa forodha ya kulinda nchi kupitia mipaka yake.
Bonanza hilo limehusisha michezo mbalimbali ya burudani na ushindani, ukiwemo mchezo wa mpira wa miguu ambapo timu ya maofisa wa TRA iliibuka washindi kwa mabao mawili kwa sifuri dhidi ya timu ya mawakala wa forodha, katika mchezo uliovuta hisia za watazamaji.
Mbali na mpira wa miguu, michezo mingine iliyochezwa ni pamoja na kuvuta kamba, kukimbiza kuku pamoja na michezo ya karata, hali iliyoleta burudani na kuimarisha mshikamano miongoni mwa washiriki.
Kamishna Mwenda amesema amefurahishwa na mwitikio wa watumishi na ubora wa michezo iliyochezwa, akisisitiza kuwa michezo ni chachu ya afya bora, umoja na utendaji kazi wenye tija.


.jpeg)



.jpeg)

.jpeg)

.jpeg)
No comments:
Post a Comment