Balozi Dkt. Aziz Mlima - mwenyekiti ya bodi ya TISEZA
MAMLAKA ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) imeendelea na kampeni yake ya kitaifa ya kuhamasisha uwekezaji wa ndani kwa kufanya Kongamano la Uwekezaji mkoani Geita, likiwa na lengo la kuwahamasisha wananchi kushiriki moja kwa moja katika shughuli za uwekezaji na kuondoa dhana potofu kuwa uwekezaji ni kwa wageni pekee.
Kongamano hilo lililofanyika leo Januari 20, 2026 katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, lilimshirikisha Mkuu wa Mkoa huo, Martine Shigela, ambaye alikuwa mgeni rasmi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Shigela aliipongeza TISEZA kwa juhudi zake za kusogeza elimu ya uwekezaji kwa wananchi wa Geita na kuwahimiza kutumia fursa zilizopo kwa kusajili miradi yao kupitia TISEZA ili kunufaika na vivutio mbalimbali vya kikodi na visivyo vya kikodi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya TISEZA, Dkt. Aziz Mlima, amesema Mkoa wa Geita una fursa nyingi za uwekezaji katika sekta mbalimbali na kusisitiza kuwa huu ni wakati sahihi kwa Watanzania kuelimishwa na kushiriki kikamilifu katika uwekezaji ili kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa na kuongeza ajira kwa wananchi.
Katika kongamano hilo, TISEZA pia ilizindua Dawati la Uhamasishaji Uwekezaji wa Ndani, ambalo linalenga kusogeza huduma za uwekezaji karibu na wananchi, kuongeza mwitikio wa Watanzania katika kuwekeza, kurahisisha utatuzi wa changamoto zinazowakabili wawekezaji, kuboresha upatikanaji wa takwimu muhimu za biashara na uwekezaji pamoja na kusimamia ardhi mahsusi kwa uwekezaji ili kuepusha migogoro na uvamizi wa ardhi.
Kwa ujumla, kongamano hilo limekuwa jukwaa muhimu la kuwawezesha wananchi wa Mkoa wa Geita kupata uelewa mpana kuhusu fursa za uwekezaji wa ndani na mchango wao katika kukuza uchumi wa taifa.
Kupitia elimu iliyotolewa pamoja na uzinduzi wa Dawati la Uhamasishaji Uwekezaji wa Ndani, TISEZA imeendelea kuthibitisha dhamira yake ya kuboresha mazingira ya uwekezaji na kuwahamasisha Watanzania kuchukua hatua za moja kwa moja katika uwekezaji.
Kampeni ya kuhamasisha uwekezaji wa ndani inatarajiwa kutekelezwa katika mikoa yote ya Tanzania Bara, ikianzia Kanda ya Ziwa watapita katika mikoa sita ambayo ni Mwanza, Geita, Mara, Bukoba, Shinyanga na Simiyu.
Pia wataendelea katika Nyanda za Juu Kusini, Kanda ya Kati, Kanda ya Kaskazini na Kanda ya Magharibi kwa kushirikiana na Wakuu wa Mikoa na Wilaya pamoja na vyombo vya habari.
Picha za pamoja.

.jpeg)


.jpeg)

.jpeg)
No comments:
Post a Comment