
Na Avila Kakingo, Michuzi Tv
MSEMAJI wa Serikali na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, imepata mafanikio makubwa katika siku 100 za uongozi wake, hususan katika maboresho na ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam, ukusanyaji wa mapato na utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati.
Akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam leo Januari 20, 2026, Msigwa amesema mkutano huo umefanyika katika Bandari ya Dar es Salaam ili kuonesha kwa vitendo kazi kubwa iliyofanywa na Serikali katika kuboresha huduma bandarini, akisisitiza kuwa bandari hiyo ni lango kuu la usafirishaji wa mizigo katika ukanda wa Afrika.
Ameeleza kuwa maboresho hayo yamelenga kuongeza ufanisi, kupunguza gharama za uendeshaji na kuiweka bandari katika ushindani wa kikanda na kimataifa.
Msigwa amesema katika mwaka wa fedha 2024/2025 bandari za Tanzania zilihudumia kiasi kikubwa cha shehena kutoka nchi jirani ikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Zambia, Rwanda, Burundi, Malawi, Uganda na Zimbabwe, jambo linaloonesha nafasi ya kimkakati ya Tanzania katika biashara ya kikanda.
Ameongeza kuwa ushiriki wa sekta binafsi kupitia mikataba kati ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na makampuni ya DP World pamoja na Tanzania East Africa Gateway Terminal Limited umeleta mabadiliko makubwa katika miundombinu na utoaji wa huduma.
Kwa mujibu wa Msigwa, ameeleza kuwa uwekezaji uliofanywa umeongeza uwezo wa Bandari ya Dar es Salaam kuhudumia shehena, ambapo katika mwaka wa fedha 2024/2025 bandari hiyo ilihudumia tani milioni 27.7, sawa na ongezeko la asilimia 17 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia.
Aidha, muda wa kuhudumia meli za makasha umepungua kwa kiasi kikubwa, hali iliyosaidia kupunguza gharama kwa wafanyabiashara na kuongeza ushindani wa bandari.
Ameongeza kuwa maboresho hayo yamechangia ongezeko la ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja pamoja na kuongeza mapato ya Serikali kupitia kodi za forodha, ambazo zimeongezeka kwa asilimia 17 katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2025.
Msigwa amesema mafanikio hayo yanaonesha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuboresha mazingira ya biashara na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Msigwa amesema kukamilika kwa miradi ya maboresho ya bandari kutaifanya Bandari ya Dar es Salaam kuwa na uwezo wa kuhudumia meli kubwa za kisasa, kuongeza uwezo wa kuhudumia shehena hadi tani milioni 30 kwa mwaka na kuimarisha ushindani wa bandari za Tanzania dhidi ya bandari nyingine katika ukanda wa Bahari ya Hindi.
Pia amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya kimkakati ili kuhakikisha bandari zinakuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.

No comments:
Post a Comment