HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, January 30, 2026

SENDIGA ASEMA HALI YA DAWA MANYARA SIYO ASILIMIA 93

Na Mwandishi Wetu, Manyara.

MKUU wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga, amepinga takwimu zinazoonesha kuwa upatikanaji wa huduma za dawa mkoani humo umefikia asilimia 93, akisema kuwa takwimu hizo haziakisi uhalisia wa hali iliyopo kutokana na wingi wa malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu ukosefu wa dawa na huduma muhimu za afya.

Sendiga ametoa kauli hiyo wakati wa kikao cha kuanza utekelezaji wa Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote (BAW) ngazi ya mkoa wa Manyara, kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, kikihusisha wadau wa afya wakiwemo Mganga Mkuu wa Mkoa, waganga wakuu wa wilaya pamoja na kamati za afya za halmashauri.

Amesisitiza kuwa utekelezaji wa bima ya afya kwa wote hauwezi kufanikiwa endapo wananchi wataendelea kukumbana na kero za ukosefu wa dawa, vipimo na huduma nyingine muhimu katika vituo vya afya na hospitali. “Huduma bora za afya lazima ziende sambamba na bima ya afya kwa wote. Wananchi hawapaswi kulalamika,” amesema RC Sendiga.

Katika kuhakikisha mpango huo unafanikiwa, Mkuu huyo wa Mkoa amezielekeza halmashauri zote za Manyara kuhakikisha zinafikisha elimu ya Bima ya Afya kwa Wote hadi ngazi ya kaya, kwa kuwafikia wananchi wa makundi yote wakiwemo vijana wa bodaboda, bajaji, wazee na kaya masikini, ili waweze kuelewa faida na umuhimu wa kujiunga na bima hiyo.

Aidha, amewataka waganga wafawidhi chini ya usimamizi wa Mganga Mkuu wa Mkoa na waganga wakuu wa wilaya kuhakikisha huduma zote muhimu, ikiwemo dawa na vipimo, zinapatikana kwa wakati katika hospitali na vituo vya kutolea huduma za afya, ili kuondoa malalamiko na kurejesha imani ya wananchi.

Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote ulianza rasmi Januari 26, 2026, ukiwa na lengo la kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma za afya kwa uhakika, nafuu na kwa usawa, hatua ambayo Mkoa wa Manyara umeanza kuitekeleza kikamilifu kwa kuhamasisha wananchi na kusimamia ubora wa huduma za afya.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad