HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, January 23, 2026

RC Queen Sendiga asogeza haki kwa wananchi, azindua kliniki za sheria bure Manyara

 

Na Mwandishi Wetu, Manyara.

MKUU wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga, amezindua rasmi kamati za ushauri wa kisheria pamoja na kliniki za sheria bila malipo zitakazotoa huduma kwa wananchi wa Mkoa wa Manyara na Wilaya zake, hatua inayolenga kusogeza huduma za haki karibu zaidi na jamii.

Uzinduzi huo umefanyika katika viwanja vya Mount Hanang Katesh, Wilaya ya Hanang, na kuhudhuriwa na viongozi wa serikali, wanasheria, wadau wa haki na wananchi mbalimbali.
 Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Sendiga amewahimiza wananchi kutumia fursa ya huduma hizo ili kutatua changamoto zao za kisheria kwa wakati na kwa njia sahihi.

Amesema kamati hizo zimeundwa kwa lengo la kutoa ushauri wa kisheria kwa wananchi, watumishi wa umma na viongozi, pamoja na kutambua changamoto za kisheria zilizopo katika jamii na kusaidia kuzitatua kabla hazijawa migogoro mikubwa.
“Kamati hizi za ushauri wa kisheria ambazo zinaanza kazi leo, zinalenga kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi wetu, lakini pia kupunguza migogoro isiyo ya lazima katika maeneo yetu,” amesema Mhe. Sendiga.

Aidha, amewataka wananchi kuacha tabia ya kutumia wanasheria wasio na sifa au watu wasiobobea katika masuala ya sheria, kwani hali hiyo imekuwa ikisababisha hasara ya muda, fedha na wakati mwingine kupoteza haki. Badala yake, amewashauri wawatumie wanasheria waliopo katika kambi za Mount Hanang na kupitia kliniki za sheria zilizoanzishwa.
Kwa upande mwingine, Mkuu wa Mkoa amezitaka kamati hizo kuendelea kuboresha utoaji wa elimu ya kisheria kwa jamii, hasa vijijini ambako bado huduma za kisheria hazijawafikia wananchi wengi. Amesisitiza pia umuhimu wa kuanzisha kliniki za sheria zinazotembea (mobile legal clinics) ili kuwafikia wananchi walioko maeneo ya mbali.

“Maelekezo ya serikali na ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha huduma zinamfikia mwananchi moja kwa moja. Hii ndiyo sababu tunaweka nguvu katika kusogeza huduma za kisheria karibu na wananchi,” aliongeza.
Wananchi waliohudhuria uzinduzi huo wameeleza kufurahishwa na mpango huo, wakisema utasaidia kupunguza migogoro ya ardhi, mirathi, ndoa na masuala mengine ya kisheria ambayo yamekuwa yakisumbua jamii kwa muda mrefu.

Mpango wa uanzishwaji wa kamati za ushauri wa kisheria na kliniki za sheria Manyara unatarajiwa kuwa chachu ya kuimarisha utawala wa sheria, kuongeza uelewa wa haki za msingi na kujenga jamii yenye haki na usawa zaidi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad