HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, January 5, 2026

NHC YATAKIWA KUJENGA NYUMBA BORA ZA GHARAMA NAFUU KWA WANANCHI WA KIPATO CHA CHINI

Na Munir Shemweta, WANMM


Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo amelitaka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kufanya utafiti wa jinsi ya kujenga nyumba bora na zenye gharama nafuu kwa wananchi wa kipato cha chini.

Dkt. Akwilapo amesema hayo leo tarehe 5 Januari 2026 wakati akizungumza na watumishi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) jijini Dar es Salaam, akiwa na Naibu wake Mhe. Kaspar Mmuya wakati wa ziara ya siku moja yenye lengo la kulifahamu shirika.


"Mfanye tafiti za jinsi ya kujenga makazi bora na kwa gharama nafuu na muelewe unafuu huo ni kwa nani, kwa kuwa kuna kada tofauti za watanzania". Amesema


"Mfanye pia tafiti za upatikanaji wa teknolojia za kisasa zitakazowezesha kupatikana kwa nyumba bora na za gharama nafuu kwa wnanchi wa kipato cha chini". Amesema Dkt Akwilapo

Kwa mujibu wa Waziri huyo wa Ardhi, kila mtanzania analiangalia shirika hilo kwa shauku kubwa kutokana na usumbufu wanaoupata wakati wa kujenga nyumba. Kunakuwa na changamoto nyingi kuanzia hatua ya ununuzi wa vifaa hadi kwa mafundi na kueleza kuwa NHC ndiyo jibu la kila kitu

Amewaambia watumishi hao wa NHC kuwa, malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) yanataka wananchi wapatiwe makazi bora, salama na na mahitaji yote muhimu, kama vile huduma za umeme na maji. Hivyo ameelekeza kwamba suala la kuwapatia watanzania makazi bora liwe kichwani mwao, hasa wakizingatia kuwa ongezeko la watu linalochochea hitaji kubwa la makazi kwa mijini.

Akigeukia utendaji kazi wa Wizara ya Ardhi, Mhe. Dkt Akwilapo amesema, wizara yake itahakikisha kuwa watumishi wa sekta ya ardhi nchini kote wanafanya kazi zao kwa weledi na kuhakikisha kuwa hakuna changamoto mpya inayotengenezwa.

"Hatutaki kuona mtumishi yeyote anatengeneza tatizo jipya na pindi tukigundua hivyo hatua kali zitachuliwa dhidi ya mhusika" amesema Dkt Akwilapo

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Kaspar Mmuya ameeleza kufurahishwa na mabadiliko ya kimfumo katika Shirika la Nyumba la Taifa.

Amewataka watumishi wa NHC kujipanga kumiliki nyumba kutokana na kuwa kwenye eneo linalohusika na nyumba.

"Nitawashangaa kukosa nyumba, Mjipange kumiliki nyumba, na uongozi uone fahari kwa kumuwekea mtu alama ya kuwa na nyumba, kila mmoja amiliki nyumba, mafanikio yawe katika sekta ya ardhi". Amesema.

Awali wakati wa kikao na Menejiment ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Mkurugenzi wa Shirika hilo Bw. Hamad Abdallah alieleza mipango, mikakati na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya shirika hilo.

Bw Hamad ameeleza kuwa, shirika lake kwa sasa linatekeleza miradi 67 yenye thamani ya bilioni 458.2 ambapo kati ya miradi hiyo ujenzi wa miradi 60 imekamilika na miradi 7 ujenzi wake uko katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

Ametaja baadhi ya miradi ikiyokamilika kuwa ni majengo 8 ya Ofisi za Wizara eneo la Mtumba jijini Dodoma, Soko la Madini (Tanzanite) lililopo Mererani, Kitengo cha Moyo Jakaya Kikwete, Ghala la Chakula- Masasi, Hospitalj ya Rufaa mkoa wa Mtwara pamoja na Shule ya Uchumi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam .

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo akizungumza na watumishi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) wakati yeye na Naibu wake Kaspar Mmuya walipotembelea shirika hilo jijini Dar es Salaam tarehe 5 Januari 2026.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo akizungumza na watumishi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) wakati yeye na Naibu wake Kaspar Mmuya walipotembelea shirika hilo jijini Dar es Salaam tarehe 5 Januari 2026. Katikati ni Naibu Waziri Kaspar Mmuya na kulia ni Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa Bw, Hamad Abdallah.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Kaspar Mmuya akizungumza na watumishi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) wakati yeye na Waziri wa Ardhi walipotembelea shirika hilo jijini Dar es Salaam tarehe 5 Januari 2026.







Sehemu ya watumishi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) wakiwa katika kikao cha Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Naibu wake kilichofanyika makao makuu ya shirika hilo jijini Dar es Salaam tarehe 5 Januari 2026.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo akipokea moja ya vitendea kazi kutoka kwa Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Bw. Hamad Abdallah (Kulia) tarehe 5 Januari 2026.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Kaspar Mmuya akipokea moja ya vitendea kazi kutoka kwa Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Bw. Hamad Abdallah (kushoto) tarehe 5 Januari 2026. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad