Katika kuadhimisha siku hiyo, Mheshimiwa Rais alipanda mti kama ishara ya kuhamasisha uhifadhi wa mazingira, ikiwa ni utekelezaji wa kaulimbiu isemayo “Uzalendo ni kutunza mazingira, shiriki kupanda miti.”
Kupitia kanda zake 13 nchini kote, NEMC imeshirikiana na wizara, taasisi za umma na binafsi, asasi za kiraia pamoja na kamati za mazingira kushiriki katika zoezi la upandaji miti katika maeneo mbalimbali yakiwemo shuleni, zahanati na katika masoko.
Akizungumza katika hafla hiyo, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu, Mkurugenzi wa Utawala na Fedha Bw. Dickson Mjinja alieleza umuhimu wa kupanda miti kama njia mojawapo ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi huku akisisitiza kuwa miti ina mchango mkubwa katika kuhifadhi ikolojia na kuboresha maisha ya binadamu.
Kwa upande wake, Meneja wa NEMC Kanda ya Ilala, Bi. Abella Muyungi, aliwataka wananchi kushiriki kikamilifu katika kusimamia na kuhifadhi mazingira nchini kwa vitendo, akisisitiza kuwa jukumu la uhifadhi wa mazingira ni la kila mmoja.
NEMC imeendelea kusisitiza dhamira yake ya kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuunga mkono juhudi za Serikali za awamu ya sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kulinda na kuhifadhi mazingira kwa maendeleo endelevu ya Taifa.
Zoezi la upandaji miti Kata ya Ilala viwanja vya msikate tamaa limeratibiwa na NEMC na Balozi wa Mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Grit Godfrey.














No comments:
Post a Comment