HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, January 17, 2026

MNARA MPYA WA AIRTEL WAIBUA FURSA ZA KIUCHUMI WILAYA YA KONGWA



KAMPUNI ya mawasiliano ya Airtel Tanzania imewahakikishia wakazi wa Wilaya ya Kongwa, Mkoa wa Dodoma, kuimarika kwa huduma za mawasiliano na intaneti baada ya kuzindua rasmi mnara mpya wa kisasa katika eneo hilo.

Uzinduzi huo uliopokelewa kwa shangwe na wananchi, viongozi wa serikali pamoja na vijana, ni sehemu ya mkakati wa Airtel wa kupanua wigo wa huduma zake na kuhakikisha maeneo ya pembezoni yanafikiwa na huduma bora za mawasiliano.

Akizungumza katika hafla hiyo, Bw. Kelvin Msumule, Mkuu wa Kitengo cha Michezo, Utamaduni na Sanaa pamoja na Maendeleo ya Vijana Wilaya ya Kongwa, amesema uzinduzi wa mnara huo ni hatua muhimu katika kuwawezesha vijana kiuchumi na kijamii kupitia matumizi ya teknolojia ya kidijitali.

“Upatikanaji wa mawasiliano bora ni nyenzo muhimu katika kukuza vipaji, biashara za vijana na ajira za kidijitali. Mnara huu unafungua fursa nyingi kwa wananchi wa Wilaya ya Kongwa,” amesema Bw. Msumule.

Kwa upande wake, Bw. Gibson Renatus, Meneja wa Airtel Kanda ya Gairo, amesema kampuni hiyo imeendelea kusikiliza mahitaji ya wateja wake na kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha huduma zinaimarika katika maeneo yenye uhitaji mkubwa.

“Airtel imejipanga kuhakikisha Watanzania wanapata huduma za uhakika.

Mnara huu ni matokeo ya maoni na maombi ya wananchi wa Wilaya ya Kongwa, na ni suluhisho la kudumu kwa changamoto za mawasiliano zilizokuwepo,” amesema Bw. Renatus.

Naye Bi. Jeni Maduma, mkazi wa Morisheni Wilayani Kongwa, ameishukuru Airtel kwa uwekezaji huo akisema kuwa utarahisisha mawasiliano, biashara ndogondogo pamoja na upatikanaji wa huduma za kifedha kupitia simu.

“Hapo awali mtandao ulikuwa changamoto kubwa, lakini sasa tuna matumaini mapya. Huu ni mwanzo mzuri wa maendeleo,” amesema Bi. Maduma.

Kwa upande wake, Bw. Baltazary Mikindo, mkazi wa Morisheni Wilayani Kongwa, amewahimiza wananchi kuulinda mnara huo ili uendelee kutoa huduma bila vikwazo.

“Miundombinu hii ni mali ya jamii. Ni jukumu letu sote kuilinda dhidi ya hujuma ili tuendelee kunufaika na huduma hizi muhimu,” amesema Bw. Mikindo.

Uzinduzi wa mnara huo umeelezwa kuja katika wakati muafaka ambapo serikali inaendelea kusisitiza matumizi ya TEHAMA katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii, huku Airtel ikionyesha dhamira ya dhati ya kuwaunganisha Watanzania kupitia huduma bora za mawasiliano.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad