HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, January 12, 2026

MIRERANI WALIA NA MAJI YA KUNYWA

 

Na Mwandishi wetu, Mirerani
WAKAZI wa mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara, kwa zaidi ya wiki moja wamelalamikia kutopata huduma ya maji ya kunywa, baada ya malori yanayouza maji hayo kutoka mji mdogo wa Boma ng'ombe wilayani Hai mkoani Kilimanjaro kudaiwa kuzuiwa.

Kwa zaidi ya miaka 20 wakazi wa mji mdogo wa Mirerani, wanatumia maji ya kunywa yanayouzwa na malori kutoka mji mdogo wa Boma ng'ombe.

Hivi sasa, baadhi ya wakazi wengine wa mji huo wanatumia maji ya visima vifupi na virefu na maji ya mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira jiji la Arusha (AUWSA) Mirerani, kwa ajili ya matumizi mengine ikiwemo kunywa.

Baadhi ya wakazi wa mji mdogo wa Mirerani, wakizungumza juu ya changamoto hiyo wameiomba serikali kuingilia kati suala hilo kwani wanatumia gharama kubwa kupata maji ya kunywa

Mmoja kati ya wakazi hao, Andrew John amesema kwa zaidi ya miaka 20 walikuwa wanatumia maji ya kunywa yanayotoka Hai ila wanasikitishwa hivi sasa kupata zuio hilo.

"Tulikuwa tunategemea malori ya kina 'Rumba Kali' kwa ajili ya kununua maji ya kunywa ila wanadai wamezuiwa kuleta maji Mirerani bila sababu ya msingi," amesema.

Amesema maji ya Hai yamewasaidia kwa muda mrefu kwani ya kisima na mengine hayakati kiu yana chumvi na maji ya chupa ni gharama kutumia na familia.

"Hivi sasa kuna baadhi ya malori machache yamefanikiwa kuleta maji Mirerani ila ndoo moja ya lita 20 ya maji ya kunywa tunauziwa Sh2,000 badala ya Sh1,000 kama awali," amesema.

Mmoja kati ya wauza maji wa eneo hilo, Abdi Soka amesema watu wengi wameathirika kwa ukosefu wa maji kutokana na zuio la mkuu wa wilaya ya Hai, Hassan Bomboko.

"Wanaoleta maji na kutuuzia kupitia malori kutoka mji mdogo wa Boma ng'ombe wamedai kuwa DC wa Hai, Hassan Bomboko amezua malori hayo yasilete maji mji mdogo wa Mirerani," amesema Soka.

Meneja wa mamlaka ya maji na usafi wa mazingira jiji la Arusha (AUWSA) Mirerani, Fidelis Shayo ameeleza kwamba hata yeye amesikia changamoto ya maji hayo kutopatikana.

Shayo amesema AUWSA aihusiki kuzuia huduma ya maji kutoka maeneo mengine japokuwa mradi wao wa maji wa Mirerani unaendelea kutoa huduma kwa uhakika maeneo hayo yakiwa safi na salama.

"Maji ya AUWSA Mirerani ni safi na salama kwani yametibiwa kwa dawa, tunaendelea kuwasihi watu wa eneo hilo waendelee kutumia hata kwa kunywa ndiyo sababu serikali imetenga Sh4.3 bilioni kwa ajili ya mradi wa maji Mirerani," amesema Shayo.

Hata hivyo, mkuu wa wilaya ya Hai, Hassan Bomboko alipoulizwa kwa njia ya simu juu ya suala hilo alikataa kulizungumzia.

"Kama upo huko Mirerani waulize viongozi wa huko juu ya suala hilo," amejibu DC Bomboko na kukata simu.

Kwa upande wake, ofisi mtendaji wa mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani (TEO) Isack Mgaya amesema kwa sababu suala hilo lipo nje ya wilaya ya Simanjiro wameshindwa kuingilia kati.

"Tulipata taarifa kuwa uongozi wa Hai ulizuia maji hayo kwa madai kuwa ni machache ila tumefikisha suala hilo kwa mkuu wa wilaya ya Simanjiro Fakii Lulandala ili azungumze na uongozi wa Hai," amesema Mgaya.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad