Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Rahma Kisuo amesema kuwa Serikali itaendelea kuunga mkono miradi yenye tija kwa maendeleo ya Taifa ikiwemo ambayo inazalisha ajira kwa vijana.
Mhe. Kisuo amesema hayo leo Januari 6, 2026 JIjini Arusha wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya Mradi wa Mount Kilimanjaro International Conventional Centre (MK- ICC) na mradi wa nyumba za makazi wa Oloirien.
Mhe. Kisuo amesema miradi hiyo ni ya kimkakati na uchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa kutoa ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kwa wananchi, hususan vijana, hivyo kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira na kuongeza kipato katika jamii zinazozunguka mradi.
Kwa upande mwengine, Naibu Waziri Kisuo ameupongeza Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kwa uwekezaji wa miradi yenye tija na maendeleo kwa Taifa.
"Ujenzi wa ukumbi mkubwa wa mikutano wa MK - ICC utakuwa na uwezo wa kuhudumia watu 5,000 kwa wakati mmoja, sambamba na kumbi ndogo za mikutano zenye uwezo wa kuhudumia watu kuanzia 50 mpaka 500, pamoja na ukumbi wenye hadhi ya Rais (Presidential summit) unaoweza kuhudumia watu 300 kwa wakati mmoja," amesema
Hali kadhalika ametoa rai kwa viongozi wa PSSSF kuendelea kuwekeza kwenye miradi yenye tija na pia kutangaza mradi huo utakapokamilika.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Fortunatus Magambo, amemuhakikishia Naibu Waziri kuwa Mfuko huo umejipanga kusimamia miradi hiyo kwa uadilifu wa hali ya juu ili kufikia malengo.
Magambo amebainisha kuwa mradi wa MK-ICC umezingatia vigezo vyote vya kisasa na unatarajiwa kuwa kichocheo kikubwa cha uchumi na utalii nchini.





No comments:
Post a Comment