HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, January 20, 2026

MAPATO YA BANDARI YAVUNJA REKODI, MSIGWA ASIFU USHIRIKIANO NA MAGEUZI YA KIDIGITALI

 

Na Avila Kakingo, Michuzi Tv
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imeandika historia mpya katika ukusanyaji wa mapato ya Bandari baada ya kuvunja rekodi ya makusanyo, hali inayotajwa kuwa matokeo ya mageuzi ya kiutendaji, matumizi ya mifumo ya kisasa ya kidigitali na kuimarika kwa ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa biashara.

Akizungumza na waandishi wa habari, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema mapato ya Bandari yameendelea kuongezeka kwa kasi katika Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kufuatia maboresho makubwa yaliyofanywa katika usimamizi wa kodi na ufanisi wa utoaji huduma.

Msigwa amebainisha hayo leo Januari 20,2026 wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Bandari ya Dar es Salaam amesema kuwa katika kipindi cha Julai hadi Desemba mwaka wa fedha 2025/26, TRA imekusanya mapato makubwa kupitia Bandari, yakichangia kwa kiasi kikubwa kufikia wastani wa makusanyo ya zaidi ya shilingi trilioni 3 (Tatu) kwa mwezi kitaifa.

Ameeleza kuwa mafanikio hayo yametokana na kuongezeka kwa shughuli za biashara bandarini, kupungua kwa ucheleweshaji wa mizigo na kuimarika kwa uwazi katika ukusanyaji wa kodi na tozo mbalimbali.

Amesema rekodi hiyo imeimarishwa zaidi mwezi Desemba 2025, ambapo makusanyo ya mapato ya Bandari yalikuwa sehemu ya mchango mkubwa uliowezesha TRA kukusanya jumla ya shilingi trilioni 4.13 kwa mwezi mmoja, kiwango ambacho hakijawahi kufikiwa hapo awali.

Kwa mujibu wa Msemaji Mkuu wa Serikali, matumizi ya Mfumo Jumuishi wa Ukusanyaji wa Mapato ya Ndani (IDRAS) yamekuwa chachu ya mafanikio hayo kwa kuwezesha ufuatiliaji wa miamala ya kikodi kwa wakati halisi, kuunganishwa kwa mifumo ya taasisi husika bandarini na kupunguza mianya ya upotevu wa mapato.

Ameongeza kuwa kupitia mfumo huo, wafanyabiashara na wakala wa forodha wanapata huduma za kikodi kwa saa 24, ikiwa ni pamoja na utoaji wa risiti za kielektroniki, uthibitishaji wa nyaraka na ukumbusho wa moja kwa moja wa majukumu ya kikodi, hatua iliyorahisisha biashara na kuongeza utii wa walipakodi.

Msigwa amesema mafanikio ya TRA katika ukusanyaji wa mapato ya Bandari ni kielelezo cha dhamira ya Serikali ya kuendelea kuboresha mazingira ya biashara, kuongeza ufanisi wa Bandari na kuhakikisha mapato ya umma yanakusanywa kwa uwazi na uadilifu kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo na huduma za kijamii.

Msigwa pia ametoa wito wa kuendeleza nidhamu ya ulipaji kodi ili Tanzania iendelee kunufaika na fursa za kiuchumi zinazotokana na Bandari zake.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad