-Atoa wito kwa viongozi wa ngazi zote za Kitaifa, kuhudhuria vikao vya Chama kwenye ngazi za Mashina.
-Asema ni mahala pa kuikusanya jamii pamoja, kutangaza kazi nzuri inayofanywa na Rais Dkt. Samia.
-Ala chakula na Mabalozi wa mashina
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt Asha-Rose Migiro, amesema Mabalozi wa Mashina ndiyo nguzo ya kukipambania Chama, kwa kuwa ni macho, masikio na daraja la kuunganisha Chama na kuendelea kulinda umoja kama nguvu ya kusonga mbele ili kuwatumikia wananchi.
Akizungumza leo, tarehe 20.1.2026 katika mkutano na Mabalozi wa Mashina Mkoa wa Dodoma, Katibu Mkuu wa CCM, Dkt Migiro, amesema Mashina ni ngome ya ulinzi wa chama, kwani yataendelea kuwa Walezi, na kuwaunganisha wananchi pamoja, na kwamba siasa lazima iende sambamba na uchumi ndio maana Mashina yana tija kwa Chama.
Amesema ni mahala pa kuikusanya jamii pamoja, kutangaza kazi nzuri inayofanywa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, huku akiwataka kufanya vikao vya mara kwa mara na kufikisha maadhimio ngazi za juu, ambapo kupitia Chama wanaweza kuishauri serikali iliyoko madarakani.
Aidha, Dkt. Migiro ametoa wito kwa viongozi wa ngazi zote za Kitaifa, kuhakikisha wanahudhuria vikao vya Chama kwenye ngazi za Mashina, ili kujadili kwa pamoja na kutatua au kueleza ahadi walizoahidi watakaposhika dola zimefikia wapi utekelezaji wake, ili kulinda umoja wa Chama na kuwa nguvu ya kusonga mbele kuwatumikia wananchi.
Awali, akitoa shukrani kwa niaba ya Wabunge waliohudhuria mkutano huo, Mbunge wa Jimbo la Mtumba na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesema katika miaka mingi iliyopita hakuna kipindi ambacho Chama kimewaangalia Mabalozi vizuri kama awamu hii ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye ni Mwenyekiti wa CCM, akitoa rai kwa Mabalozi na viongozi wote kuyafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa na Katibu Mkuu wa CCM.






















No comments:
Post a Comment