Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo, amekabidhi jumla ya vifaa vya TEHAMA 1,429 vyenye thamani ya Shilingi Bilioni 5.2 kwa ajili ya Ofisi za Ardhi katika halmashauri 184 nchini, pamoja na ofisi za Makamishna wa Ardhi Wasaidizi wa Mikoa.Makabidhiano hayo yamefanyika tarehe 23 Januari, 2026, jijini Dodoma, wakati wa kikao kazi kati ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na watumishi wa sekta ya ardhi pamoja na wale wa taasisi zilizo chini ya Wizara.
Vifaa vilivyokabidhiwa ni juhudi ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuhakikisha huduma katika sekta ya ardhi zinaimarishwa na kuboreshwa kwa ofisi za ardhi kupatiwa vifaa ili kurahisisha utendaji kazi wao katika kuwahudumia wananchi.
Vifaa vya TEHAMA vilivyokabidhiwa ni Kompyuta za kawaida 424, Kompyuta zenye uwezo mkubwa kwa ajili ya kazi za ardhi (GIS computer) 250, Skrini za Kusomea Ramani (GIS display) 391, Skana 41, Printa 44, Simu za Mezani zinazotumia Mtandao wa Taasisi bila kulipia (IP phones) 82, pamoja na UPS 197.
Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo, amesema Wizara yake imefanya maboresho mbalimbali ya kisera na kiutendaji, ikiwemo mifumo kidijiti ya utoaji wa huduma za sekta ya ardhi.
Amesisitiza kuwa, Wizara yake haitavumilia ucheleweshaji wowote wa utoaji huduma kwa wananchi kwa visingizio vya kukosa vitendea kazi.
Hata hivyo, amewataka watendaji hao wa sekta ya ardhi nchini, kuhakikisha vifaa hivyo vinatunzwa sambamba na kuzingatia matumizi ya mifumo ya TEHAMA iliyopo kwa lengo la kuhakikisha huduma zinatolewa kwa ufanisi.
Moja ya vipaumbele vya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi katika Bajeti ya Mwaka 2025/2026 ni kuimarisha mifumo ya TEHAMA katika utunzaji wa kumbukumbu, utoaji wa huduma, ukusanyaji wa maduhuli, na upatikanaji wa taarifa za ardhi na uthamini.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo akimkabidhi vifaa vya TEHAMA kwa ajili ya kazi za sekta ya Ardhi Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Mtwara Bw. Fredrick Mrema wakati wa Kikao Kazi kati ya Waziri wa Ardhi na Watumishi wa Sekta ya Ardhi tarehe 23 Januari, 2026 jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Kaspar Mmuya akimkabidhi vifaa vya TEHAMA Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Lindi Geofrey Martin wakati wa Kikao Kazi kati ya Waziri wa Ardhi na Watumishi wa Sekta ya Ardhi tarehe 23 Januari, 2026 jijini Dodoma.

No comments:
Post a Comment