Na Farida Mangube Morogoro
Katika hatua ya kuimarisha nafasi ya mtoto wa kike katika elimu na uchumi wa Taifa, Shirika lisilo la kiserikali la CAMFED limeandika historia baada ya kufanikiwa kusomesha na kuwawezesha kiuchumi wasichana zaidi ya laki moja kutoka mikoa 10 ya Tanzania, huku zaidi ya wasichana 34,000 wakinufaika ndani ya mwaka mmoja pekee wa 2025.
Akizungumza katika maadhimisho ya mafanikio ya mwaka 2025 ya mtandao wa CAMA , Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa CAMFED, Anna Sawaki, amesema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano wa karibu kati ya CAMFED na Serikali kupitia taasisi zake ikiwemo VETA, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Vijana, SIDO pamoja na Halmashauri, katika kuwaandaa wasichana kupata elimu, ujuzi wa ufundi, mikopo na fursa za kujitegemea kiuchumi.
Amesema maadhimisho hayo yaliwakutanisha wanachama wa Mtandao wa wasichana walionufaika na ufadhili wa masomo wa CAMFED (CAMA), ambapo wasichana hao walipata nafasi ya kuonesha shughuli mbalimbali za uzalishaji mali walizozianzisha baada ya kuhitimu mafunzo ya ufundi stadi. Shughuli hizo ni pamoja na ushonaji, useremala, ufundi wa chuma na shughuli nyingine zinazolenga kuongeza thamani ya bidhaa na mazao yao.
Anna ameeleza kuwa baadhi ya wasichana walidhaminiwa moja kwa moja na CAMFED, huku wengine wakisomeshwa kupitia ushirikiano kati ya CAMFED, wadau wa maendeleo pamoja na Halmashauri ambapo kupitia mafunzo hayo wanufaika wamepata ujuzi uliowawezesha kuongeza thamani ya bidhaa wanazozalisha na kupanua masoko yao.
Katika kuendeleza uwezeshwaji huo, mtandao wa wahitimu wa CAMFED unaojulikana kama CAMA umeendelea kuwa mhimili muhimu wa kusaidia watoto na vijana wa kike katika jamii ambapo kwa mujibu wa CAMFED hadi sasa mtandao huo una wanachama takribani 83,000, huku kwa mwaka 2025 pekee ukifanikiwa kuwafikia watoto wengine zaidi ya laki 110 wenye uhitaji mkubwa katika Halmashauri 35 za mikoa 10.
Ameongeza kuwa maadhimisho hayo yalikuwa na lengo la kusherehekea mafanikio yaliyopatikana, lakini pia kuwasilisha ujumbe kwa Serikali na wadau wa maendeleo kuwa bado kuna hitaji kubwa la kuwaunganisha wasichana hao na masoko, mitaji na teknolojia za kuongeza thamani ya bidhaa na mazao yao.
“Lengo letu ni kumfanya mtoto wa kike aweze kujitegemea yeye mwenyewe, kuisaidia familia yake na hatimaye kuleta mabadiliko chanya katika jamii kwa ujumla,” amesema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtandao wa CAMA, Shamsa Mkuruno, amesema mtandao huo umefanikiwa kusaidia watoto zaidi ya laki moja na elfu 14, ikiwemo kuwarejesha shuleni wanafunzi waliokatiza masomo kutokana na changamoto mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
Ameongeza kuwa wanachama 511 wa CAMA wamepata mikopo isiyo na riba kutoka CAMFED, hatua iliyowawezesha kukuza biashara zao pamoja na kupata ruzuku za kuanzisha miradi mipya ya kiuchumi, ambapo idadi kubwa yao ilifanikiwa kuanzisha biashara mwaka 2025.
Mbali na biashara, amesema wanachama wengi wa mtandao huo wanajishughulisha na kilimo bora kwa kutumia mbegu bora na teknolojia ya kisasa, hatua inayoongeza kipato cha kaya na kuchochea maendeleo endelevu katika jamii zao.





No comments:
Post a Comment