Na. OWM-KAM, Dar es Salaam
Serikali ya Awamu ya Sita imesema inajivunia ushirikiano wa kidugu ulipo kati yake na Taifa la Qatar ambao umesaidia kukuza diplomasia ya uchumi na upatikanaji wa ajira.
Kauli hiyo ya Serikali imetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Ajira na Mahusiano Deus Sangu wakati wa hafla ya kuadhimisha siku ya Taifa la Qatar iliyofanyika katika hoteli ya Johari Rotana Dar es Salaam 04 Desemba 2025.
Waziri Sangu aliongeza kusema Tanzania na Qatar zimeendelea kuwa na mahusiano chanya kwa miaka mingi ambapo sekta za biashara, uwekezaji, utalii, elimu na ajira zimepata mafanikio.
Kuhusu sekta ya ajira Waziri Sangu alitaja mafanikio hayo ni pamoja na kampuni ya MOWASALAT ya Qatar kuajili watanzania 800 kwa kazi ya udereva mwezi Mei 2025 na nafasi zingine 1,092 mwezi Septemba 2025 hatua inaonesha matunda ya ushirikiano.
Kuhusu sekta ya utalii, Waziri Sangu alisema jumla ya watalii 496 kutoka Qatar walitembelea Tanzania mwaka 2024 kwa mujibu wa Jarida la Takwimu Tanzania na kwamba serikali iko katika hatua za mwisho kukamilisha mkataba wa makubaliano ya kukuza sekta ya utalii.
Waziri Sangu alieleza kuwa Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan anathamini ushirikiano baina ya mataifa hayo mawili na kwamba atatumisha ili uzidi kuchangia ukuaji wa uchumi na kuboresha maisha ya watu.
Kwa upande wake Balozi wa Qatar nchini Tanzania Fahad Rashid Al Marekhi alisema siku ya uhuru wa Taifa hilo inaadhimishwa ili kuenzi historia na mafanikio yaliyofikiwa ikiwemo utekelezaji wa Dira ya maendeleo ya mwaka 2030.
Balozi Al Marekhi aliongeza kusema Serikali ya Qatar itaendelea kuwa mshirika wa maendeleo kwa Tanzania kwa kusaidia uwekezaji kwenye miundombinu, usafiri, michezo na huduma za kijamii.
Kuhusu ushiriki wa Qatar kwenye uupatanishi wa migogoro duniani, Balozi Al Marekhi alitaja mafanikio yaliyopatikana kwa uongozi wa nchi hiyo kuwezesha usuluhishi wa mgogoro wa Gaza, Mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Ulaya kupitia njia ya mazungumzo yanayosimamiwa na nchi yake.
Hafla hiyo ya Siku ya Taifa la Qatar ilihudhuriwa na Mabalozi na wawakilishi wa nchi na Serikali toka mataifa mbalimbali wenye makazi yao Dar es Salaam pamoja na viongozi wa Serikali ya Tanzania na raia wa Qatar wanaoishi nchini Tanzania.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi, Ajira na Mahusiano Mheshimiwa Deus Sangu (kulia) akipokea zawadi kutoka kwa Balozi wa Qatari nchini Tanzania Mheshimiwa Fahadi Rashid Al Marekhi (kushoto) jana (04 Desemba 2025) wakati wa hafla ya kuadhimisha Siku ya Taifa la Qatar iliyofanyika Johari Rotana Dar es Salaam ambapo Waziri Sangu alikuwa mgeni rasmi.
Picha ya pamoja ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Ajira na Mahusiano Mheshimiwa Deus Sangu akiwa na Mabalozi wanaowakilisha nchi zao nchini Tanzania wakati wa hafla ya Siku ya Taifa la Qatar jana hoteli ya Johari Rotana Dar es Salaam
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi, Ajira na Mahusiano Mheshimiwa Deus Sangu (kulia) akiwa kwenye mazungumzo na Balozi wa Qatari nchini Tanzania Mheshimiwa Fahadi Rashid Al Marekhi (kushoto) jana (04 Desemba 2025) wakati wa hafla ya kuadhimisha Siku ya Taifa la Qatar iliyofanyika Johari Rotana Dar es Salaam ambapo Waziri Sangu alikuwa mgeni rasmi.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi, Ajira na Mahusiano Mheshimiwa Deus Sangu (kulia) akiwa kwenye mazungumzo na Makamu Mwenyekiti Msataafu wa CCM Taifa Ndugu Abdulrahman Kinana (kushoto) jana (04 Desemba 2025) wakati wa hafla ya kuadhimisha Siku ya Taifa la Qatar iliyofanyika Johari Rotana Dar es Salaam






No comments:
Post a Comment