HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, December 18, 2025

WAZIRI AKWILAPO AAGIZA KUONGEZWA KWA KASI YA KUPANGA NA KUPIMA ARDHI NCHINI

Na Munir Shemweta, WANMM


Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo ameiagiza Tume ya Taifa ya Matumizi ya Ardhi kuongeza kasi ya kupanga na kupima ardhi katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo miradi ya kilimo, makazi na uwekezaji.

Mhe. Dkt Leonard Akwilapo amesema hayo leo tarehe 17 Desemba 2025 wakati akifungua Kikao Kazi cha Kamati ya Ufundi ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi kilichofanyika Makao Makuu ya Wizara jijini Dodoma.

Kupitia kikao hicho, Mhe. Dkt Akwilapo amehimiza kukuzwa kwa matumizi ya teknolojia katika ukusanyaji takwimu za kupanga ardhi, kulinda maeneo nyeti ya ikolojia, misitu, vyanzo vya maji, njia za wanyama pori pamoja na kujenga ustahimilivu wa mabadiliko ya tabia nchi kupitia mipango shirikishi na endelevu,

Amesema,Tanzania inakabiliwa na changamoto zinazohusiana na matumizi ya ardhi na kuzitaja kuwa ni pamoja na migongano kati ya shughuli za kilimo na ufugaji, malisho na uhifadhi na upungufu wa maeneo ya uwekezaji wa kimkakati kutokana na mabadiliko ya matumizi ya ardhi yasiyopangwa.

Changamoto nyingine ni uharibifu wa mazingira unaosababishwa na uvamizi wa vyanzo vya maji, ukataji miti hovyo, matumizi ya ardhi yasiyo rasmi, mabadiliko ya tabia nchi yanayoongeza shinikizo kwa ardhi na rasilimali zake na ukuaji wa haraka wa miji unaohitaji mipango bunifu na matumizi bora ya ardhi.

Katika kukabiliana na changamoto hizo, Mhe Dkt Akwilapo amesema, Serikali inategemea utaalamu na ushauri wa Kamati ya Ufundi ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi katika kuhakikisha ardhi inatumika kwa tija, usawa, usalama na uendelevu.

"Ninaamini ushauri wa Kamati utakuwa mhimili wa kuimarisha Sera, miongozi na taratibu zinazohusu matumizi ya ardhi nchini". Amesema Mhe. Dkt Akwilapo

"Niielekeze Tume kuwa makini kusaidia kamati kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi. Muwasidie ili waweze kutekeleza majukumu ili kusiwe na migongano mbele ya safari". Amesema.

Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhandisi Anthony Sanga Amesema, wizara yake ina imani kubwa na kazi za Tume ya Taifa ya Matumizi ya Ardhi kutokana na kuisaidia wizara na hasa katika maeneo ya migogoro ya vijijni ikiwemo ya wakulima na wafugaji.

"Nikiri kuwa migogoro ya wakulima na wafugaji imepungua sana tofauti na ilivyokuwa miaka ya zamani maana tulikuwa na kesi nyingi za hii migogoro lakini kwa kiasi kikubwa imepungua".Amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) Bw. Joseph Mafuru amesema,Tume yake itahakikisha kamati inatekeleza majukumu yake kwa weledi huku akiamini wajumbe walioteuliwa wataziwakilisha vyema taasisi walizotoka kwa kutekeleza kikamilifu majukumu ya Kamati.

"Katika kipindi chote ambacho Tume imekuwa bila Kamati, tumekosa mambo kadhaa muhimu kama vile fursa ya kupata ushauri wa kitaalamu unaotekelezwa kimfumo na kitaalamu katika sekta zote kuhusiana na matumizi ya ardhi kuanzia kilimo, mifugo, misitu, utalii, ujenzi, uwekezaji na nyinginezo ikiwemo tafiti". Amesema

Kwa mujibu wa Bw. Mafuru, mambo mengine ni kukosekana kwa mkakati wa pamoja wa utanzaji wa migogoro ya ardhi, upungufu wa takwimu za pamoja, pengo la uratibu wa taasisi pamoja na upungufu wa viwango vya kitaifa vya mipango.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo akizungumza wakati wa kufungua Kikao Kazi cha Kamati ya Ufundi ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi kilichofanyika Makao Makuu ya Wizara jijini Dodoma tarehe 17 Desemba 2025.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo akimkabidhi vitendea kazi mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Ufundi ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi Bw. Joseph Osena wakati wa Kikao kazi cha Kamati hiyo kilichofanyika jijini Dodoma. Kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Mhandisi Anthony Sanga.




Sehemu ya Washiriki wa kikao kazi cha Kamati ya Ufundi ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi kilichofanyika Makao Makuu ya Wizara jijini Dodoma tarehe 17 Desemba 2025.
Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Matumizi ya Ardhi Bw. Joseph Mafuru akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha Kamati ya Ufundi ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi kilichofanyika Makao Makuu ya Wizara jijini Dodoma tarehe 17 Desemba 2025.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo (katikati mstari wa mbele) akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa kamati ya ufundi ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi mara baada ya kufungua kikao kazi cha Kamati hiyo jijini Dodoma tarehe 17 Desemba 2025. Wa kwanza kushoto mstari wa mbele ni Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Mhandisi Anthony Sanga na kulia ni Mkurugenzi mkuu wa Tume ya Taifa ya Matumizi ya Ardhi Bw. Joseph Mafuru.(PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad