.jpeg)
Waumini wa Kanisa Katoliki nchini Tanzania, Stanslaus Thobias Nyakunga na Elia Phaustine Kabote, wakizungumza kuhusiana na kupeleka Barua kwa Balozi wa Vatican nchini Tanzania juu ya Mwenendo wa Katibu wa TEC Dkt.Charles Kitima jijini Dar es Salaam.
Na Mwandishi Wetu
WAUMINI wa Kanisa Katoliki nchini Tanzania, Stanslaus Thobias Nyakunga na Elia Phaustine Kabote, wamewasilisha rasmi barua kwa Archbishop Angelo Accattino, Balozi wa Vatican nchini, wakiomba kufanyika kwa uchunguzi wa kichungaji na kiutawala kuhusu mwenendo wa Padri Dkt. Charles Kitima, Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC).
Kwa mujibu wa waumini hao, hatua hiyo imechukuliwa kufuatia malalamiko na mitazamo iliyoenea kwa muda mrefu katika jamii, kwamba Padri Kitima kuhusishwa na masuala ya siasa yanayoendelea kuonekana kuingilia kutokana na matamko yake.
Waumini hao wanasema mitazamo hiyo, iwe ni ya kweli au la, imeanza kuibua sintofahamu miongoni mwa waumini na kuliweka Kanisa katika mazingira yanayoweza kutafsiriwa kama ya upendeleo wa kisiasa, hali inayohatarisha nafasi ya Kanisa kama taasisi ya amani, upatanisho na mwongozo wa kimaadili kwa jamii.
Katika barua yao kwa Balozi wa Vatican, Nyakunga na Kabote wamesisitiza kuwa hawakusudii kutoa hukumu wala kumshambulia mtu binafsi, bali wanaiomba mamlaka ya Kanisa kulishughulikia suala hilo kwa busara ya kichungaji ili kulinda umoja wa waumini na taswira ya Kanisa.
Waumini hao wamerejea pia Maandiko Matakatifu wakisisitiza wajibu wa viongozi wa Kanisa kuwa nguzo za amani na maridhiano, wakinukuu kauli ya Biblia inayosema “Heri wapatanishi, maana hao wataitwa wana wa Mungu” (Mathayo 5:9), pamoja na “Kwa maana Mungu si wa machafuko bali wa amani” (1 Wakorintho 14:33). Aidha, wametaja onyo la Mtume Paulo dhidi ya mgawanyiko miongoni mwa waumini (1 Wakorintho 1:10).
Hatua hiyo ya waumini inakuja katika kipindi ambacho taifa linapitia mjadala mpana wa kisiasa na kijamii, ambapo taasisi za dini zinatarajiwa kuwa nguzo za utulivu, maridhiano na mshikamano wa kitaifa, badala ya kuonekana kuvutwa katika mvutano wa vyama.
Katika barua yao, waumini hao wameomba mambo matatu makuu: kufanyika kwa uchunguzi wa mwenendo wa Padri Kitima, kutolewa kwa mwelekeo wa wazi unaohakikisha uongozi wa Kanisa unabaki huru dhidi ya siasa za vyama, na kuchukuliwa kwa hatua zozote zitakazolinda umoja wa waumini, amani ya jamii na mamlaka ya kimaadili ya Kanisa.
Waumini hao wamesema wanaamini kuwa na busara na mamlaka ya kushughulikia suala hilo kwa maslahi mapana ya Kanisa na jamii kwa ujumla.

No comments:
Post a Comment