HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, December 9, 2025

WANAFUAIKA WENYE ULEMAVU WAELEZA JINSI TASAF ILIVYOBADILISHA MAISHA YAO

Na Said Mwishehe,Michuzi TV

WAKATI leo Desemba 9,2025 Watanzania wanasherehekea miaka 64 ya uhuru ni wazi kumekuwepo na hatua mbalimbali za kuendelea kutokomeza umasikini,ujinga na maradhi.

Katika kutokomeza umasikini,ujinga na maradhi, Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) umeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuhalikisha inawakomboa wananchi hasa wanaotoka kaya masikini na miongoni mwao wakiwemo watu wenye ulemavu ambao Desemba 3 mwaka huu wameadhimisha siku ya Watu wenye ulemavu duniani.

Hata hivyo leo Disemba 9 wakati Watanzania wakisherehekea miaka 64 ya Uhuru, TASAF nayo inasherehekea mafanikio makubwa ya kuboresha maisha ya wananchi walio wengi hasa zilizokuwa kaya masikini.

Juhudi hizo za TASAF zinalenga katika kuendeleza mapambano yaliyoasisiwa na Baba wa Taifa na Rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere za kupambana na maadui watatu, maradhi, umasikini na ujinga.

Ni wazi kwamba Mfuko huo umekuwa ukitoa ruzuku kwa walengwa mbalimbali wakiwemo watu wenye ulemavu kwa kuwapa ruzuku na fedha za uzalishaji mali ili kupambana na adui umasikini.

Kupitia mfuko wa TASAF, Maalim Kesi (60) ambaye ni mlemavu wa macho kutoka kijiji cha Kaole, Bagamoyo mkoani Pwani ni mmoja wa wanufaika ambaye anaeleza kwamba hajui ni namna gani angeweza kusomesha watoto wake kama si TASAF.

Amefafanua kuwa ana watoto tisa, na kati ya hao, watoto sita walikuwa kwenye mpango wa TASAF na walipata msaada mkubwa uliomuwezesha kuwasomesha na kuwapatia mahitaji ya muhimu.

“Nawashukuru sana TASAF. Fedha nilizokuwa napokea nakumbuka ni kati ya 40,000 mpaka 50,000 zilinisaidia sana kuinua maisha yangu, siwezi kusahau,”anasema Kesi.

Pamoja na hayo amesema anamshukuru Rais wa Tanzania wa Awamu ya Sita, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza kwa vitendo maono ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere katika kuondoa ujinga, umasikini na maradhi.

Pia ametoa pongezi kwa uongozi wa TASAF, kwa namna wanawasaidia wanufaika.

Kwa upande wake mlemavu, Latifa Mshindo (42) wa kijiji cha Kondo, Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani, amesema TASAF imemsaidia kuinuka kiuchumi pamoja na kumsaidia kusomesha watoto wake na kuwapatia mahitaji muhimu nyumbani na shuleni.

Amesema aliingia kwenye mpango wa TASAF akiwa na maisha ya chini sana, na yeye ni mlemavu ambaye hana mkono mmoja, maisha yake yalikuwa magumu na ilimlazimu kukaa nyumbani kwa wazazi mpaka pale alipoanza kunufaika na mpango wa TASAF.

“Nilianza kwa kupewa ruzuku ya Sh. 17,000 kwa mwezi ambayo baadae iliongezeka kufikia 22,000 fedha hizi pamoja na zile ambazo nilikuwa nalipwa kwa kufanya shughuli mbalimbali kwenye miradi ya TASAF ambapo nilikuwa nalipwa 30,000, kwa pamoja zilinisaidia kuboresha biashara yangu ya samaki ambayo nilianza na mtaji wa shilingi 7,000 lakini mpaka nahitimu TASAF nimekuwa na mtaji wa zaidia ya 100,000.”

Akiendelea, Bi. Latifa, alisema bado anaendelea na biashara yake ya kuuza samaki na kwa sasa ameongeza meza ya pili ikiashiria ongezeko la mtaji na mali katika biashara yake.

Aidha amesema mbali na fedha hizo, pia alipata fursa ya kupata mafunzo ya ujasiriamali kutoka kwa wataalam wa TASAF na baada ya kumaliza alipata fedha za uzalishaji mali (350,000).

Amesisitiza kupitia TASAF ameweza kujenga nyumba ambayo kwa sasa ipo kwenye hatua za mwisho, lakini pia Mfuko huo umemsaidia kusomesha watoto wake.

“Najivunia kuwa sehemu ya wanafuika wa TASAF na hapa ninapozungumza nafurahi kuona mtoto wangu wa kwanza amemaliza chuo cha ufundi na mwingine yuko kidato cha tatu akiendelea na masomo.

Wakati Watanzania tunasherehekea miaka 64 tangu tupate Uhuru, ukweli ni kwamba tunaona fahari nchi yetu kupitia TASAF ikiendelea kubadilisha maisha ya wananchi waliyo na hali duni kiuchumi na leo kama mimi sio tegemezi tena,nina shughuli nazofanya kupata kipato.”

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad