HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, December 29, 2025

Ujenzi wa Makavazi ya Muungano ipo ukingoni

 


Mwandishi Wetu, Unguja

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni amesema ahadi iliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya ujenzi wa kituo cha kumbukumbu na Nyaraka za Muungano (Makavazi) inaelekea ukingoni.

Mhe. Masauni amesema hayo Disemba 28, 2025 wakati wa Uwekaji wa Jiwe la Msingi Jengo la Taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu Zanzibar ambapo mgeni rasmi alikuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla kuelekea shamrashamra za miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Amesema Mhe. Dkt. Samia alipokuwa Mnazi Mmoja, Zanzibar kwenye kampeni ya uchaguzi moja ya ahadi alizotoa ndani ya miaka mitano atakayofanya ni pamoja na ujenzi wa Makavazi ya Muungano ambapo yatakuwepo Dodoma, Dar es Salaam na Zanzibar.

“Nichukue fursa hii Mgeni rasmi kuwaelezea wananchi kwamba ahadi hiyo ya Mhe. Rais ya ujenzi wa makavazi inaelekea ukingoni, na hivi karibuni nilipata nafasi ya kutembelea jengo lililopo pale Dodoma na kwa kuanzia tutaanza na Dar es Salaam kwa kutumia kwa muda ukumbi wa Karimjee kisha Zanzibar,” amesema Mhe. Masauni.

Ameongeza kuwa makavazi hayo yatasaidia vijana kupata elimu baada ya kugundua kuna vijana wengi bado hawana uelewa wa kutosha kuhusu mambo yanayohusu Muungano na historia ya nchi.

Amesisitiza kuwa moja ya mkakati wa utoaji wa elimu kwa umma kuhusu mambo yanayohusu Muungano, Ofisi ya Makamu wa Rais itahakikisha matumizi sahihi ya makavazi hiyo.

Mh. Masauni amesema kwenye makavazi hayo kutakuwa na uhifadhi wa vitu mbalimbali ambapo wananchi watakuwa wanakwenda kuona na kujifunza, hivyo uwepo wa Taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu Zanzibar na Makavazi itakuwa suluhisho kwa wengi kujua historia ya nchi.

Maeneo yaliyopendekezwa katika makavazi hiyo ni pamoja na sehemu ya kuhifadhi nyaraka, eneo la kupokelea nyaraka, eneo la uhifadhi nyaraka, eneo la kusomea, ukumbi wa mikutano, eneo la makumbusho na eneo la utawala.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad