Akizungumza wakati wa kupokea tuzo hiyo jijini Dar es Salaam, Mjumbe wa Bodi ya TPDC, Mrisho Shabani, aliyemwakilisha Mwenyekiti wa Bodi, alisema matokeo hayo yanaonesha mipango madhubuti na dhamira ya uwajibikaji.
“Hatujaingia kwenye mashindano haya kama watazamaji. Huu ulikuwa ni ushiriki wetu wa kwanza, na kumaliza katika nafasi ya pili kunadhihirisha maandalizi na nidhamu yetu,” alisema.
Bw. Shabani alisema tuzo hiyo imeongeza morali kwa watumishi wa TPDC, hususan wahasibu, na kwamba heshima hiyo itaharakisha maboresho katika uandaaji wa taarifa na utendaji kazi.
“Tunajivunia mafanikio haya, lakini pia yanatupa changamoto ya kurekebisha mapungufu ili kurejea tukiwa imara zaidi,” aliongeza.
Aidha, alisema TPDC inaendelea kuboresha miundombinu ya gesi asilia ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya watumiaji wa CNG, viwanda na kaya.
“Tunapoboreshaji mifumo yetu, uzalishaji utaongezeka na wateja wengi zaidi wataweza kupata gesi asilia kwa uhakika mkubwa,” alisema.
Akifunga hafla hiyo, Naibu Waziri wa Fedha, Laurent Deogratius Luswetula, alisema tuzo hizo ni nguzo muhimu ya uwajibikaji na utawala bora nchini.
“Uwasilishaji bora wa taarifa za fedha ni muhimu kwa walipa kodi, wawekezaji na washirika wa maendeleo wanaotegemea taarifa sahihi kufanya maamuzi,” alisema.
Aliipongeza Mkutano wa Mwaka wa Wahasibu 2025 kwa kuangazia mustakabali wa taaluma hiyo, akisisitiza kuwa wahasibu wana nafasi muhimu katika kusimamia rasilimali za taifa.
“Kazi yenu ni msingi wa uthabiti wa uchumi wa Tanzania na ustahimilivu wa muda mrefu,” alisema.
Mkurugenzi Mkuu wa NBAA, CPA Pius Aloysius Maneno, alisema mashindano ya mwaka huu yalizingatia viwango madhubuti vya uchambuzi na tathmini.
“Kila taarifa iliyowasilishwa ilipitia hatua mbili za uchambuzi kwa kuzingatia viwango vya kimataifa, maoni safi ya ukaguzi na matakwa ya utawala bora,” alisema, akibainisha kuwa orodha ya viwango waliotumia ilikuwa wazi kwa umma ili kuongeza uwazi.
“Utaratibu huu unaimarisha imani katika mfumo wa uwasilishaji taarifa za fedha nchini na kukuza utamaduni wa uadilifu,” aliongeza.
Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) ilitangazwa mshindi wa kwanza katika kundi la taasisi za serikali, huku TPDC ikishika nafasi ya pili.



No comments:
Post a Comment