
SERIKALI imeeleza dhamira yake ya kusogeza huduma karibu na wananchi na kuongeza uwazi katika ajira za umma kupitia matumizi ya teknolojia ya kidijitali, hatua inayolenga kupunguza urasimu na gharama kwa waombaji wa ajira na wapokeaji wa huduma za Serikali.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, amesema Serikali imeanza tathmini ya rasilimali watu katika taasisi za umma ili kuhakikisha mahitaji halisi ya watumishi yanazingatiwa kwa haki na weledi.
Amesema tathmini hiyo itawezesha Serikali kujenga mfumo wa ajira unaozingatia ushindani, uwajibikaji na ufanisi, sambamba na kutekeleza ahadi ya kuongeza ajira kwa Watanzania, hususan katika sekta za afya na elimu.
Kwa mujibu wa Waziri Ridhiwani, mchakato mpya wa ajira utaanza Desemba 13, 2025, ambapo kwa mara ya kwanza usaili utafanyika katika mikoa yote nchini kwa kutumia mfumo wa mtandaoni wa online aptitude test, hatua itakayopunguza gharama na usumbufu kwa waombaji.
Katika kuimarisha mawasiliano kati ya Serikali na wananchi, Waziri huyo amezindua rasmi mfumo wa Mrejesho unaopatikana kwa kupiga 15400#, utakaomwezesha mwananchi kutoa maoni, malalamiko au pongezi moja kwa moja kwa viongozi na taasisi za umma bila vikwazo.
Aidha, amesema kuanzishwa kwa Daftari la Huduma za Serikali (GSD) kutawawezesha wananchi kupata taarifa sahihi za huduma, gharama na taratibu bila kulazimika kufika ofisini, hivyo kuongeza uwazi na kuokoa muda.
Akizungumzia masuala ya maadili, Ridhiwani amesema Serikali ipo katika hatua za kurekebisha sheria za maadili ya viongozi na watumishi wa umma ili kuimarisha uwajibikaji na uadilifu katika ngazi zote.
Amesisitiza kuwa licha ya changamoto za awali za mifumo mipya, Serikali imelenga kufikisha zaidi ya asilimia 80 ya huduma zote za umma kwenye mifumo ya kidijitali ifikapo mwaka 2050, kama sehemu ya mkakati wa kujenga Serikali inayowajibika na inayomlenga mwananchi.

No comments:
Post a Comment