HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, December 8, 2025

SERIKALI YATANGAZA VIPAUMBELE VIPYA VYA UWEKEZAJI NA FURSA KWA VIJANA KUELEKEA UTEKELEZAJI WA DIRA 2050

 

Na Avila Kakingo, Michuzi Tv
SERIKALI kupitia Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji imetaja vipaumbele vyake vikuu katika sekta ya uwekezaji kwa kipindi cha miaka mitano ijayo, ikiwa ni hatua muhimu kuelekea utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar Es Salaam leo, Desemba 8, 2025, amesema Serikali imejipanga kutoa nafasi kubwa kwa vijana, kuongeza ajira, na kuvutia mitaji mikubwa ya maendeleo.

Akizungumza kuhusu mafanikio yaliyopatikana kati ya mwaka 2021 na 2025, Waziri Mkumbo amesema miradi ya uwekezaji imeongezeka kutoka 252 hadi 901 kwa mwaka, huku mtaji ulioingia nchini ukipanda kutoka Dola Bilioni 3.7 mwaka 2021 hadi Dola Bilioni 9.3 mwaka 2024.

Ameongeza kuwa katika kipindi cha 2025–2030 Serikali itaendelea kuimarisha Kituo cha Mahala Pamoja (One Stop Facilitation Centre) chenye taasisi 14 ili kupunguza urasimu na kuongeza ufanisi katika utoaji huduma kwa wawekezaji.

Amebainisha kuwa kipaumbele kitaelekezwa katika sekta 10 muhimu ikiwemo kilimo na uchakataji, uzalishaji wa bidhaa tunazoagiza kutoka nje (kama mafuta ya kupikia, ngano na dawa), ufugaji, uvuvi, utalii, ujenzi, madini, misitu, nishati, na huduma za fedha.

Aidha, Serikali inazindua Benki ya Ardhi yenye zaidi ya hekta 170,000 kwa ajili ya uwekezaji, pamoja na kuanzisha Jukwaa la Kitaifa la Uwekezaji litakaloanza Januari 2026 kwa ajili ya kufanya tathmini ya mara kwa mara na kusikiliza changamoto za wawekezaji.

Akizungumzia mkakati mahsusi wa kuwawezesha vijana, Prof. Mkumbo amesema serikali itaanzisha Kituo Maalum cha Wawekezaji Vijana, na kutenga maeneo ya ardhi katika mikoa ya Dodoma, Pwani, Mara, Ruvuma na Bagamoyo ili vijana waanzishe viwanda na miradi ya uzalishaji.

" Kupitia mpango huu, vijana watapewa mafunzo, kuunganishwa na benki, kupata mitambo, malighafi na miundombinu ya msingi inayohitajika kuanzisha biashara zenye tija." Amesema

Prof. Mkumbo ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji kupitia Mpango mpya wa MKUMBI utakaozinduliwa kabla ya kuanza rasmi kwa utekelezaji wa Dira 2050 mnamo Julai 2026. Vilevile, maandalizi ya mpango wa kwanza wa miaka mitano na mpango wa mwaka mmoja (2026/2027) yanaendelea, sambamba na mfumo mpya wa ufuatiliaji na upimaji wa matokeo (RBMELA-Framework).

Ameeleza kuwa serikali pia imekamilisha maandalizi ya muswada wa sheria mpya ya uwekezaji wa umma ambayo italeta mageuzi katika usimamizi wa mashirika ya umma, ikiwemo kuongeza uwazi wa uteuzi wa viongozi, kuhamasisha mashirika kujiandikisha kwenye soko la hisa na kuweka mfumo mpya wa upimaji tija.

Akihitimisha, Waziri Mkumbo amesema Serikali ya Awamu ya Sita inalenga ifikapo mwaka 2030 iwe imezalisha ajira milioni nane, kuvutia mitaji angalau Dola Bilioni 50, kuimarisha usimamizi wa miradi ya maendeleo na kuongeza tija ya mashirika ya umma katika kutoa huduma kwa wananchi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad