HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, December 22, 2025

Serikali Yaendelea Kuwezesha Wafanyabiashara Ndogondogo Kupitia Mikopo Nafuu ya NMB

 


Na Avila Kakingo, Michuzi Tv
SERIKALI imeendelea kuchukua hatua madhubuti za kuwawezesha wafanyabiashara ndogondogo, hususan vijana na wanawake, kwa kutoa mikopo yenye masharti nafuu kupitia Benki ya NMB, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kukuza uchumi wa wananchi na kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira nchini.

Akizungumza leo Desemba 22, 2025 jijini Dar es Salaam wakati wa kutoa taarifa kwa umma kuhusu utekelezaji wa shughuli za maendeleo na fursa kwa makundi maalum kwa mwaka wa fedha 2025/26, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, amesema mikopo hiyo inalenga kuwawezesha wafanyabiashara ndogondogo kuongeza mitaji, kukuza biashara na kuongeza ushiriki wao katika shughuli za kiuchumi.

Dkt. Gwajima ameeleza kuwa Serikali kupitia Wizara yake, kwa kushirikiana na Benki ya NMB, imeweka mfumo wa utoaji mikopo yenye riba nafuu ya asilimia saba (7%), ili kuhakikisha wafanyabiashara wadogo wanapata fursa ya mitaji kwa urahisi zaidi na kwa masharti rafiki ukilinganisha na mikopo ya kibiashara ya kawaida.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, hadi sasa jumla ya wafanyabiashara ndogondogo 4,870 wamenufaika na mikopo yenye thamani ya shilingi 9.9 bilioni, fedha ambazo zimetumika kuimarisha biashara mbalimbali zikiwemo za huduma, uzalishaji na biashara ndogondogo katika maeneo ya mijini na vijijini.

Amesisitiza kuwa mikopo hiyo imelenga kwa kiasi kikubwa vijana na wanawake ambao ndio kundi kubwa la wafanyabiashara ndogondogo nchini, akibainisha kuwa uwezeshaji wa makundi hayo ni nguzo muhimu katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na jitihada za Serikali za kujenga uchumi shindani na jumuishi.

Dkt. Gwajima ametoa wito kwa wafanyabiashara ndogondogo ambao bado hawajanufaika na mikopo hiyo kujitokeza na kujisajili katika mfumo wa Wafanyabiashara Ndogondogo Management Information System (WBN-MIS) kupitia Maafisa Maendeleo ya Jamii katika Halmashauri zao, ili waweze kupata taarifa sahihi na kunufaika na fursa zilizopo.

Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kuboresha mifumo ya uwezeshaji kiuchumi kwa kushirikiana na taasisi za kifedha ili kuhakikisha wafanyabiashara ndogondogo wanapata mikopo kwa wakati, kwa masharti nafuu na kwa uwazi, hatua itakayochochea ukuaji wa biashara, kuongeza ajira na kuinua kipato cha wananchi.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad