MFAMASIA Jackson Mahagi (39) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashtaka ya wizi wa dawa na vifaa vya hospitali vyenye thamani ya Sh bilioni tisa mali ya MSD.
Mahagi ambaye ni Mfamasia wa Halmashauri ya Wilaya ya Momba mkoani Songwe amesomewa mashtaka yake mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya na Wakili wa serikali, Frank Rimoy.
Akisoma hati ya mashtaka Wakili Rimoy, alidai mshitakiwa anakabiliwa na mashitaka matatu na katika shtaka la kwanza ambalo ni wizi akiwa mtumishi inadaiwa mshitakiwa alitenda kosa hilo kati ya Januari 2021 na Aprili,2025 eneo la Keko Mwanga, Dar es Salaam na Chitete wilaya ya Momba mkoani Songwe.
Inadaiwa kuwa katika tarehe hizo mshitakiwa akiwa mfamasia aliiba dawa na vifaa vya kusambazwa katika hospitali mbalimbali kutoka MSD ambavyo vilikabidhiwa kwake,vyote vikiwa na thamani ya Sh bilioni tisa
Katika shitaka la pili inadaiwa kuwa kipindi hicho hicho mshtakiwa akiwa mkoani Songwe alisababishia MSD hasara ya Sh bilioni tisa.
Pia katika shtaka la tatu la utakatishaji fedha, inadaiwa mshtakiwa alijipatia kiasi hicho cha fedha huku akijua kuwa fedha hizo ni zao la kosa tangulizi la wizi.
Hatahivyo, mshitakiwa hakurusiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi ya Uhujumu Uchumi.
“Kwa mujibu wa hati ya mashitaka anakabiliwa na makosa ya uhujumu uchumi na Mahakama hii haina mamlaka ya kusikiliza shauri hili na shitaka la tatu unalaokabiliwa nalo ni la utakatishaji huwezi kupewa dhamana hata Mahakama kuu,” alisema hakimu Lyamuya.
Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kesi imeahirishwa hadi Desema 16,mwaka huu kwa ajili ya kutajwa kwa njia ya mtandao na kuamuru mshitakiwa arudishwe rumande.


No comments:
Post a Comment