Mbunge wa Jimbo la Nachingwea, Fadhili Liwaka,akisonga ugali kwenye moja ya masoko ambayo mama nitilie wanaojihusisha na uuzaji wa vyakula

Mbunge wa Jimbo la Nachingwea, Fadhili Liwaka,akisonga ugali kwenye moja ya masoko ambayo mama nitilie wanaojihusisha na uuzaji wa vyakula.
Mbunge wa Jimbo la Nachingwea, Fadhili Liwaka, amewahakikishia mama lishe wa jimbo hilo kuwa atashughulikia changamoto zinazowakabili zikiwemo upatikanaji wa maji safi, usafi wa masoko, mikopo kwa wajasiriamali wadogo pamoja na maboresho ya miundombinu ya masoko ili yawe rafiki kwa wafanyabiashara na wateja.
Na Fredy Mgunda, Nachingwea.
MBUNGE wa Jimbo la Nachingwea, Fadhili Liwaka, amewahakikishia mama lishe wa jimbo hilo kuwa atashughulikia changamoto zinazowakabili zikiwemo upatikanaji wa maji safi, usafi wa masoko, mikopo kwa wajasiriamali wadogo pamoja na maboresho ya miundombinu ya masoko ili yawe rafiki kwa wafanyabiashara na wateja.
Mheshimiwa Liwaka ametoa ahadi hiyo wakati wa ziara ya mikutano mbalimbali na mamalishe katika Kata za Nachingwea na Ugawaji, ikiwa ni sehemu ya jitihada zake za kuimarisha ushirikiano na kusikiliza kero zao moja kwa moja.
Akizungumza katika Soko Kuu la Nachingwea, Mbunge Liwaka alisema ameanza ziara zake kwa wajasiriamali wadogo kutokana na kutambua mchango wao mkubwa katika kuendesha uchumi wa familia na jamii kwa ujumla. Alisisitiza kuwa mamalishe ni nguzo muhimu ya uchumi wa chini, hivyo wanastahili kupewa kipaumbele.
“Ni wajibu wangu kuwa karibu nanyi, kuwashukuru kwa kuniunga mkono katika Uchaguzi Mkuu na kuomba ushirikiano wenu katika kuendelea kulijenga Jimbo la Nachingwea,” alisema Mheshimiwa Liwaka.
Kwa upande wake, mmoja wa mamalishe wa Soko la Voda, Bi. Fortunata Robert Makarius, alimpongeza Mbunge huyo kwa kuwafuata uso kwa uso, akisema hatua hiyo imewapa faraja na matumaini makubwa kwani haijawahi kufanywa na mbunge yeyote aliyewahi kuliongoza jimbo hilo.
Mbunge Liwaka alimalizia kwa kuwahakikishia mamalishe kuwa Serikali ya Wilaya kwa kushirikiana na Halmashauri itaendelea kushughulikia changamoto zao kwa hatua, huku akisisitiza mshikamano na ushirikiano kama msingi muhimu wa maendeleo ya Jimbo la Nachingwea.


No comments:
Post a Comment