HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, December 16, 2025

MAKAMU WA RAIS AWEKA JIWE LA MSINGI KAMPASI YA UDSM KAGERA

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi amesema kuwa sekta ya Elimu, hususan elimu ya Juu ina mchango mkubwa katika uchumi wa Taifa, kutokana na kuzalisha nguvukazi inayoshiriki kutoa huduma katika sekta mbalimbali.

Mhe. Nchimbi ametoa kauli hiyo Disemba 15, 2025 Mkoani Kagera baada ya kuweka Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Kampasi ya Kagera ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kutokana na mchango huo, Serikali imejizatiti kuleta mageuzi ya elimu katika ngazi zote, ili kuhakikisha kuwa wahitimu wanapata ujuzi, stadi na maarifa yanayoendana na soko la ajira.

"Rai yangu kwa UDSM, hakikisheni Kampasi hii mpya inakuwa kitovu cha uvumbuzi na ubunifu; kuwawezesha vijana wetu kuibua mawazo mapya, kufanya ubunifu, na kutumia fursa za soko la pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki’’ Amesema Dkt. Nchimbi.

Mhe. Nchimbi ameipongeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kuratibu mradi mkubwa wa HEET kwa kuhakikisha matumizi adili ya fedha na kwa kuzingatia thamani ya fedha.

Ameitaka Wizara kushirikiana na wadau kuandaa mapema mahitaji kama vile ithibati, vifaa na rasilimaliwatu, ili kuwezesha shughuli za mafunzo katika Kampasi hiyo kuanza kama ilivyopangwa bila kuchelewa

Pia ameipongeza UDSM, kwa kusimamia mchakato wa ujenzi wa Kampasi hiyo, ameitaka kuendelea kuwa mfano wa kuigwa katika matumizi bora ya rasilimali na utoaji wa elimu yenye tija kwa kizazi cha leo na kesho.

"Hapa niwatake wasimamizi mkabdarasi na wote wanauhusika kuhakikisha ujenzi unakamilika kwa wakati uliopangwa hatutavumilia ucheleqaji wowote". Amesema

Ameishukuru Benki ya Dunia kwa kushikiriana na Serikali kufadhili utekelezaji wa mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), ambao umewezesha ujenzi wa Kampasi ya Kagera hukua akiahidi uwekezaji katika kukamilisha jengo la abweni la wanafunzi wa kiume na miundombinu mingine muhimu.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam na Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete amesema kuwepo kwa Chuo hicho kutakuwa kichocheo cha fursa za kiuchumi na uwekezaji wa Mkoa wa Kagera.

"Nimeambiwa bei ya viwanja na ardhi katika maeneo yanayozunguka Chuo imepanda maradufu. Lakini pia kutakuwepo na mahitaji ya Hosteli kwa wanafunzi na nyumba za kupanga kwa wafanyakazi wa Chuo.
Nawaomba ndugu zangu Wanabukoba mchangamkie fursa hizo". Amesema Dkt. kikwete.

Aidha ameeleza kuwa Chuo hicho kinaanza kama Kampasi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam lakini matumaini yetu ni kuwa siku za usoni kampasi hiyo inaweza kuja kuwa Chuo Kikuu ambapo akatolea mfano Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili (MUHAS) na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) navyo vilianza kama Kampasi za Chuo Kikuu cha Dar es Salaam lakini leo hii ni Vyuo Vikuu vinavyojitegemea.

"Imekuwa hivyo kwa MUHAS na SUA kutokana na nia ya dhati ya Serikali kuendelea kuwekeza na kuwezesha Kampasi hizo kukua na kutanuka. Naamini na sina shaka kuwa itakuwa hivyo kwa Kampasi hii pia, miaka ijayo". Ameeleza.

Naye Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda amesema ujenzi wa Kampasi ya Kagera utaongeza fursa za udahili kwa wanafunzi, kuchochea ukuaji wa uchumi wa eneo husika na kuimarisha matumizi ya teknolojia pamoja na tafiti katika Kanda ya Ziwa.

Waziri Mkenda amesema kampasi hiyo inatarajiwa kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya elimu na sekta za uzalishaji.

Amesema Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) ni mradi mkubwa wa kimkakati unaolenga kubadilisha mfumo mzima wa elimu ya juu nchini na kuufanya kuwa injini ya uchumi wa kisasa.


















No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad