HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, December 28, 2025

DC Ilala Aagiza Polisi Kuwakamata Wauaji wa Salehe Iddi Salehe



Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, ameliagiza Jeshi la Polisi Wilaya ya Kipolisi Ilala, kupitia Kamanda wake ACP Yustino Mgonja, kuhakikisha linawakamata mara moja watu wote waliohusika na mauaji ya kikatili ya mwananchi Salehe Iddi Salehe.

Marehemu Salehe Iddi Salehe alivamiwa nyumbani kwake katika Mtaa wa Zavala, Kata ya Buyuni, Jijini Dar es Salaam, tarehe 04 Desemba, 2025, majira ya saa 11 alfajiri, na kundi la watu wasiojulikana wanaodaiwa kuwa wahalifu. Baada ya kushambuliwa kikatili, alifariki dunia siku hiyo hiyo akiwa njiani akipelekwa Hospitali ya Amana, majira ya saa 2 asubuhi.

Akizungumza katika mkutano wa wananchi wa Mtaa wa Zavala, DC Mpogolo alisema marehemu alikuwa mzalendo wa kweli aliyepigania kwa muda mrefu kulinda maeneo ya wazi ya Serikali, ikiwemo ardhi za shule, masoko na vituo vya afya, dhidi ya genge la wahalifu waliokuwa wakiyauza kinyume cha sheria.

Alifafanua kuwa maeneo hayo ni sehemu ya viwanja vilivyopimwa na Serikali kupitia Programu ya Viwanja 20,000 katika Kata ya Buyuni kati ya miaka 2003 hadi 2005, ambapo marehemu alikuwa mstari wa mbele kupinga uvamizi na uuzwaji wa maeneo ya umma.

Mpogolo aliongeza kuwa Jeshi la Polisi, chini ya uongozi wa ACP Mgonja, lina mifumo na nyenzo madhubuti za kiuchunguzi na ukamataji, hivyo aliwataka wananchi kuliamini Jeshi hilo ili kurejesha hali ya usalama na kuimarisha utawala wa sheria katika Wilaya ya Ilala.

Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya alimwagiza Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, kupitia Idara ya Mipango, kuendelea kubaini, kutambua na kurejesha maeneo yote ya wazi ya huduma za jamii yaliyotengwa na kulipiwa na Serikali.

Pia alisisitiza kuwepo kwa ushirikiano wa karibu kati ya Jiji la Dar es Salaam na Jeshi la Polisi ili kubaini na kuvunja genge la wahalifu wa ardhi wanaouza viwanja vya umma kwa wananchi wasio na uelewa wa kisheria.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad