HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, December 10, 2025

Benki ya CRDBB Yatwaa Tuzo ya Mshindi wa Jumla kwa Uwasilishaji Bora wa Taarifa za Fedha Tuzo za NBAA


Dar es Salaam, Tanzania — Benki ya CRDB imethibitisha kwa mara nyingine tena uongozi na ubora wake katika utayarishaji wa taarifa za fedha baada ya kutunukiwa Tuzo ya Mshindi wa Jumla kwa Uwasilishaji Bora wa Taarifa za Fedha kwa mwaka 2024. Tuzo hii ya heshima hutolewa na Bodi ya Taifa ya Uhasibu na Ukaguzi (NBAA) kwa taasisi zinazowasilisha taarifa za fedha zenye ubora wa kimataifa na zinazoendana kikamilifu na viwango vya kimataifa vya uhasibu (IFRS).

Mbali na ushindi huo wa jumla, Benki ya CRDB pia imeibuka Mshindi wa Kwanza katika sekta ya taasisi za fedha, ikidhihirisha tena nafasi yake kama taasisi inayoongoza kwa uwazi, weledi na uadilifu katika usimamizi wa taarifa zake za kifedha.

Hafla ya utoaji wa tuzo hizo imefanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa APC Hotel, Bunju, jijini Dar es Salaam, na kuhudhuriwa na wataalamu na viongozi mbalimbali kutoka taasisi za umma na binafsi.

Akiwasilisha tuzo hizo kwa Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya CRDB, Bw. Frederick Nshekanabo, Naibu Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Laurent Deogratius Luswetula, aliipongeza Benki ya CRDB kwa kuendelea kuwa kielelezo cha ubora katika maandalizi ya taarifa za fedha. 


Alisema maandalizi ya taarifa sahihi, zinazoendana na viwango vya kitaifa na kimataifa, ni msingi muhimu unaowawezesha wawekezaji, mamlaka za usimamizi na wananchi kutathmini ufanisi, uwajibikaji na uimara wa taasisi husika katika usimamizi wa rasilimali.

“Hii ni mara ya sita mfululizo kwa Benki ya CRDB kutwaa tuzo hizi. Hii si tu rekodi ya ndani bali ni ishara ya uthabiti na dhamira ya dhati ya benki kutoa taarifa za kifedha kwa kiwango cha juu cha uwazi na uwajibikaji,” alisema Mheshimiwa Luswetula.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hizo, Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya CRDB, Bw. Frederick Nshekanabo, alisema: “Tuzo hizi ni ushahidi wa mifumo madhubuti ya usimamizi wa taarifa za fedha inayozingatia viwango vya kimatifa ndani ya Benki yetu ya CRDB. Tunajivunia kuendelea kutambuliwa katika tuzo hizi kwani inaendelea kujenga imani kwa wawekezaji, wateja na wadau wote kupitia taarifa sahihi, za kuaminika na zinazozingatia viwango vya kimataifa. Utambuzi huu unatupa nguvu zaidi ya kuendelea kuwekeza katika mifumo, watu na utawala bora.”

Bw. Nshekanabo aliongeza kuwa Benki ya CRDB inaendelea kuipa kipaumbele ahadi ya uwazi na uwajibikaji, ikiitumia kama nguzo ya kukuza uaminifu na kuimarisha uthabiti wa taasisi hiyo katika soko la fedha. Alisema kuwa misingi hiyo imekuwa dira ya benki katika miaka yote, ikiongoza maboresho ya mifumo ya ndani, matumizi ya teknolojia bunifu na uimarishaji wa utamaduni wa weledi miongoni mwa watumishi. 

Kwa kuendelea kuweka uwazi mbele, Benki ya CRDB inaendelea kuthibitisha kuwa taasisi za kifedha zinaweza kutoa huduma za kisasa huku zikidumisha viwango vya juu vya kimaadili na uadilifu wa taarifa.

Tuzo hizi, kwa mujibu wa uongozi wa Benki ya CRDB, ni matokeo ya kazi ya pamoja inayohusisha timu nzima ya benki kuanzia ngazi ya bodi, menejimenti hadi watumishi wa kawaida ambao kwa pamoja wanajenga misingi imara ya utoaji taarifa sahihi. 
Benki imesisitiza kuwa itaendeleza mafunzo, uwekezaji katika teknolojia na uimarishaji wa mifumo ya uthibiti ili kuhakikisha inaendelea kuwa mstari wa mbele katika uwasilishaji wa taarifa za kifedha zinazotegemewa ndani na nje ya nchi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad