Na Veronica Mrema, Pretoria
Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu wa Afrika Kusini, Profesa Blade Nzimande, amesema Bara la Afrika linahitaji kwa kiwango kikubwa waandishi wa habari waliobobea katika masuala ya sayansi ili kusaidia kukuza ubunifu, tafiti na maendeleo kwa ujumla.
Akizungumza wakati akifungua rasmi Mkutano wa 13 wa Waandishi wa Habari za Sayansi Duniani (WCSJ2025) unaofanyika Pretoria kuanzia Desemba 1–5, Prof. Nzimande alisema uandishi wa sayansi ni daraja muhimu kati ya wanasayansi na jamii, na umuhimu wake ni mkubwa kuliko wakati mwingine wowote.
“Sayansi haimaanishi chochote kama haiwezi kufahamika kwa jamii,” alisema. “Waandishi wa habari ni daraja muhimu la kuileta sayansi kwa watu, lakini ni daraja lenye haki ya kuikosoa pale inapostahili. Afrika bado tunahitaji waandishi wengi mahiri wa uandishi wa sayansi.”
Amesema bara hilo lina mikakati mikubwa kama Mkakati wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu wa Afrika (STISA 2034), lakini utekelezaji wake unategemea pia uwepo wa mawasiliano imara na weledi wa waandishi wa habari.
Kupambana na dhana potofu na taarifa za uongo
Waziri huyo ameeleza kuwa waandishi wa habari wana jukumu la kupambana na dhana potofu, ubaguzi na taarifa za uongo (fake news), hasa katika enzi ambayo mitandao ya kijamii inatawala mawasiliano.
“Mitandao ya kijamii imeleta faida, lakini pia imekuwa chanzo kikubwa cha kusambaa kwa taarifa zisizo sahihi. Wakati wa COVID tumeshuhudia madhara yake. Madai kama chanjo kusababisha autism ni mifano ya hatari tunazopaswa kupambana nazo,” alisema, akiwataka waandishi kuwa jasiri kuuliza maswali makubwa na muhimu.

Umuhimu wa AI katika uandishi wa habari za sayansi
Prof. Nzimande alisema teknolojia ya akili bandia (AI) ni lazima ipewe nafasi katika sekta ya habari ili kuboresha weledi na uwazi wa taarifa, huku akiitaka Afrika kuongeza ushiriki katika masuala ya kisayansi duniani.
“Hatuwezi kuachwa nyuma. Tunahitaji kuingiza AI katika uandishi wa sayansi na kutatua pengo la namna Afrika inavyoripotiwa katika sayansi,” alisema.
Diplomasia ya sayansi na nafasi ya waandishi
Ameeleza kuwa sayansi haina mipaka, hivyo ina nafasi kubwa katika kuimarisha diplomasia kati ya mataifa. Ameongeza kuwa waandishi wa habari za sayansi ni sehemu muhimu katika kufanikisha malengo ya kitaifa na kikanda ya kukuza ushirikiano wa kisayansi.
“Bila ninyi, hatuwezi kuwafikia wale tunaopaswa kuwafikia. Nyinyi ni washirika muhimu katika kuifanya sayansi ifikike kwa watu wote,” alisema.
Mkutano wa WCSJ2025 unaendelea kujadili changamoto na mustakabali wa uandishi wa sayansi barani Afrika na duniani, huku ukilenga kuongeza uelewa, uthabiti na mchango wa sayansi katika maendeleo ya kijamii.



No comments:
Post a Comment