HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, November 28, 2025

Waziri Kitila Azindua Bodi ya TISEZA, Aweka Mwelekeo Mpya wa Uwekezaji na Ajira kwa Vijana

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, akizungumza jijini Dar es Salaam leo Novemba 28, 2025, wakati wa hafla ya uzinduzi wa bodi ya TISEZA pamoja na mwongozo kwa wawekezaji ambapo ni utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ambayo inataka kujenga uchumi jumuishi, shindani na wenye mazingira wezeshi kwa biashara na uwekezaji.
Mkurugenzi  Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA), Bw. Gilead Teri akizungumza jijini Dar es Salaam leo Novemba 28, 2025 wakati wa Uzinduzi wa Bodi ya TISEZA na Mwongozo kwa wawekezaji.

Na Avila Kakingo, Michuzi Tv
SERIKALI imezindua rasmi Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA), pamoja na Mwongozo wa Watoa Huduma kwa Wawekezaji (ISPs), hatua inayoashiria mwanzo wa mageuzi mapana katika sekta ya uwekezaji nchini.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Novemba 28, 2025, wakati wa hafla hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, amesema uzinduzi wa bodi hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ambayo inataka kujenga uchumi jumuishi, shindani na wenye mazingira wezeshi kwa biashara na uwekezaji.

Waziri Mkumbo amebainisha kuwa TISEZA, iliyoanzishwa chini ya Sheria ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi ya 2025, ndio chombo kikuu cha kuratibu na kuendeleza uwekezaji nchini, ikichukua nafasi ya TIC na EPZA zilizounganishwa.

Amesema TISEZA inapaswa kuwa injini ya kutafsiri maono ya Dira 2050 katika kuvutia wawekezaji, kuboresha mazingira ya biashara na kuijenga Tanzania kuwa miongoni mwa nchi tatu bora barani Afrika kwa urahisi wa kufanya biashara.

“Jukumu la TISEZA ni kubadilisha ndoto za Taifa kuwa vitendo. Mwekezaji akifika TISEZA anatakiwa kumaliza changamoto zake zote hii ndiyo maana ya huduma mahala pamoja,” amesisitiza.

Akizungumzia fursa kwa vijana, Waziri Mkumbo ametangaza mikakati mipya ya kuvutia uwekezaji na kupanua fursa za ajira kwa vijana, ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa Kituo Maalum cha Wawekezaji Vijana (Youth Investors Resource Centre) kitakachotoa mafunzo, ushauri na uwezeshaji kwa vijana wanaotaka kuwekeza.

Pili ni kuwa na Programu ya Taifa ya Uwekezaji wa Viwanda kwa Vijana, ikiwa ni pamoja na kutenga maeneo ya ardhi kwa vijana wanaomaliza vyuo kuanzisha viwanda. Maeneo yaliyotengwa ni Dodoma (Nala, ekari 100), Pwani (Kwala, ekari 20), Mara (Bunda, ekari 100), Ruvuma (Songea, ekari 100) na Bagamoyo (ekari 20).

Tatu ni kupanua huduma za TISEZA hadi kila mkoa kufikia 2028, sambamba na agizo la Rais Samia la kusogeza huduma kwa wananchi.

Nne ni Ubia na sekta binafsi kujenga miundombinu ya viwanda kupitia ujenzi wa "industry shades" kwa gharama nafuu kwa Watanzania.

Tano ni kuanzisha vivutio vipya vya uwekezaji mara kwa mara, ikiwemo kusikiliza maoni ya wawekezaji kupitia jukwaa maalum litakaloanzishwa Januari 2026.

Aidha, ametangaza mpango maalum wa kuendeleza Eneo Maalum la Kiuchumi Bagamoyo, ili litumike kama kitovu kipya cha viwanda na biashara mara baada ya ujenzi wa bandari kukamilika.

Waziri Mkumbo amesema serikali inakamilisha Mkakati wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji (MKUMBI II) ambao utaondoa vikwazo vinavyokwamisha biashara na uwekezaji.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa TISEZA kuendelea kushauri Serikali kuhusu maeneo yenye tija ikiwemo uzalishaji wa bidhaa zinazotumia fedha nyingi kuagizwa kutoka nje, kama vile mafuta ya kula na ngano.

Katika hitimisho la hotuba yake, Prof. Mkumbo ameitaka TISEZA kuhakikisha inalifikia lengo la kusajili miradi angalau 1,500 na kuvutia mitaji ya dola bilioni 15 katika mwaka wa fedha 2025/26.

“Tanzania ni salama kwa uwekezaji. Changamoto zilizojitokeza ni nafasi ya kujijenga na kuimarika zaidi. Nawaamini  kazi kwenu!” amesema.

Pia Prof. Mkumbo amewashukuru viongozi na wawekezaji waliohudhuria na kusisitiza dhamira ya serikali ya kuimarisha sekta ya uwekezaji kwa kasi zaidi, sambamba na uteuzi wake mpya. 

Kwa Upande wa Mkurugenzi  Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA), Gilead Teri amesema kuwa mwongozo kwa watoa huduma kwa wawekezaji ambao ambao umezinduliwa leo utawasaidia wawekezaji kwenye shughuli zao.

"Tumeamua kuwaleta pamoja chini ya mwamvuli mmoja wa Mamlaka, tuwape leseni tuweze kuwapa mafunzo na  kuhakikisha huduma wanazozitoa kwa wawekezaji ziko sawa zinaendana na sheria, lakini pia  hatuharibii taswira nzima ya nchi."

Amesema wadau hao namna moja wapo ya kuwawezesha lakini pia kuwadhibiti ili kuhakikisha kuwa hakuna utapeli au kuharibu taswira ya nchi kutokana na wale wanaowahudumia wawekezaji.



Matukio mbalimbali wakati wa Uzinduzi wa Bodi ya TISEZA na Mwongozo kwa wawekezaji.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad