

KAMPUNI ya Kamal kupitia Kamal Foundation imeonesha mfano wa namna ushirikiano kati ya sekta binafsi, Serikali na jumuiya za kimataifa unavyoweza kuleta matokeo chanya kwa watu wenye ulemavu, baada ya kugawa miguu bandia kwa walengwa 28 jijini Dar es Salaam—hatua inayotajwa kuunga mkono ajenda ya kitaifa ya kuongeza ujumuishwaji katika maendeleo.
Akizungumza katika tukio hilo leo Novemba 16, 2025, Mbunge wa Viti Maalumu kwa kundi la watu wenye ulemavu, Stella Ikupa, amesema misaada kama hii inaonesha namna sekta binafsi inavyoweza kuchangia juhudi za Serikali katika kuongeza ushiriki wa watu wenye ulemavu kwenye shughuli za kiuchumi. Amehimiza kuendelezwa kwa ushirikiano wa aina hiyo ili huduma ziwafikie hata walioko mikoani pamoja na kutoa fursa za ajira kwa walengwa.
Mkurugenzi Mkuu wa Kamal Foundation, Sameer Gupta, amesema hatua hiyo ni sehemu ya dhamira ya kampuni kushirikiana na Serikali katika kuboresha ustawi wa wananchi kupitia programu endelevu za kijamii. Amebainisha kuwa wanatambua ukubwa wa changamoto wanazopitia watu wanaopoteza viungo, hivyo wataendelea kushirikiana na wadau kufikisha huduma hiyo nchi nzima.
Akitoa mtazamo wa kimataifa, Mkurugenzi wa Global Compact ya Umoja wa Mataifa, Masha Makatayambi, amesema taasisi za ulinzi na huduma za dharura—ikiwemo Jeshi la Polisi—zina wajibu wa kujiunga na majukwaa ya kimataifa yanayoboresha huduma kwa watu waliokumbana na majanga na ulemavu. Amesema zaidi ya watu milioni 30 duniani wanahitaji viungo bandia, huku Tanzania ikikabiliwa na uhitaji kwa zaidi ya watu 600,000, idadi inayoongezeka kutokana na ajali, hasa za bodaboda.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Temeke, John Malulu, amesema Kamal Foundation imekuwa mshirika muhimu wa jeshi hilo kwa kuwapongeza na kuwajengea motisha askari wanaofanya vizuri na kutoa misaada ya kijamii, hatua inayochochea ushirikiano baina ya taasisi za usalama na wadau wa maendeleo.

No comments:
Post a Comment