HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, November 13, 2025

TBS Yazindua Shindano la Uandishi wa Insha kwa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limezindua shindano la uandishi wa insha kwa wanafunzi wa vyuo vikuu nchini, ikiwa ni sehemu ya maandalizi kuelekea maadhimisho ya Siku ya Viwango Barani Afrika, yenye lengo la kukuza uelewa na ushiriki wa vijana katika masuala ya ubora wa viwango.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Novemba 13, 2025, Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Ashura Katunzi, amesema mashindano hayo yanalenga kuwahamasisha wanafunzi kuelewa nafasi ya viwango katika kukuza maendeleo endelevu ya uchumi wa viwanda na biashara nchini.

“Washindi watakaopatikana katika shindano hili hawataishia kushindana nchini pekee, bali watapata nafasi ya kushiriki katika shindano lingine la bara la Afrika litakalofanyika Machi 2026,” alisema Dkt. Katunzi.

Ameongeza kuwa ushiriki wa TBS katika maadhimisho ya Siku ya Viwango Barani Afrika ni hatua muhimu inayowezesha taasisi hiyo kujifunza na kubadilishana uzoefu na wataalamu pamoja na wadau kutoka mataifa mbalimbali, jambo linalosaidia kupanua wigo wa bidhaa za Tanzania kuingia na kukubalika katika masoko ya nje.

Aidha, Dkt. Katunzi ameishukuru serikali kwa kuendelea kuweka mazingira wezeshi ya biashara, pamoja na kuboresha mifumo ya uratibu na usimamizi wa mipango, ili kuhakikisha nchi inafikia malengo ya maendeleo endelevu kupitia ujenzi wa uchumi wa viwanda.

“Tunafahamu kuwa viwango ni nguzo muhimu katika kukuza sekta ya viwanda. Tunavitumia kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa nchini zinakuwa na ubora na usalama unaohitajika, iwe ni bidhaa za ndani au zile zinazoagizwa kutoka nje,” amesema.

Vilevile, ametoa pongezi kwa wadau mbalimbali wakiwemo taasisi za elimu, watafiti, wazalishaji, wajasiriamali na wadau wa maendeleo kwa mchango wao katika kuboresha na kuandaa viwango vinavyosaidia kuimarisha sekta ya viwanda na biashara nchini.

Dkt. Katunzi amehitimisha kwa kutoa wito kwa wananchi na wadau kushiriki kikamilifu katika maandalizi ya viwango vya bidhaa, ili kuhakikisha vinakidhi mahitaji ya jamii na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika soko la kimataifa.

Maadhimisho ya mwaka huu ya Siku ya Viwango Barani Afrika yamebeba kaulimbiu isemayo: “Nafasi ya viwango vilivyoainishwa katika kupunguza vikwazo vya kiufundi vya biashara katika kukuza biashara ya haki na usawa ndani ya Bara la Afrika na kimataifa.”








No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad