WAZIRI wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo (Mb) amefanya ziara ya kwanza ya kikazi na kuongea na wananchi wa Halmashauri ya Mji Makambako, Kata ya Maguvani katika Soko la Matema na Kata ya Mji Mwema katika Soko la Nyanya, mkoani Njombe tarehe 28 Novemba 2025.
Wakulima hao wanaojishughulisha na kilimo biashara wameeleza kwa Waziri Chongolo changamoto za miundombinu katika masoko, kuuziwa mbolea na mbegu feki na uhitaji wa teknolojia ya kuhifadhi mazao ili yasiharibike kabla ya kuwafikia wanunuzi wa ndani na nje ya nchi. Wameeleza kuwa pamoja na nyanya za Makambako kuwa soko kubwa nchini pia wameeleza kuwa wanauza nyanya nchini Zambia, Malawi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Kongo (Congo DRC).
Katika hotuba yake, Waziri Chongolo ameeleza kuwa “ukiwa kiongozi jifunze kuwa mkweli… sema jambo ambalo una uhakika kulitimiza.” Ameongeza kuwa alitoa ahadi kuanza kutatua kero na leo amelipatia soko la Matema mifuko ya saruji 500 kwa ajili ya kukarabati soko, vyoo na kizimba cha kuhifadhia taka ndani ya siku 14.
Kwa upande wa soko la Mji Mwema, Waziri Chongolo ameelekeza wataalamu kutoka Wizara ya Kilimo kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA), Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA), Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) na Wadau katika mnyororo wa thamani wa kilimo kutatua changamoto za Soko hilo zikiwemo utafutaji wa masoko ndani na nje ya nchi, teknolojia ya kuhifadhi nyanya ili zisiharibike, teknolojia za uongezaji wa thamani ya zao hilo, na upatikanaji wa mbegu na mbolea zenye ubora.
Amewahakikishia kuwa changamoto zao zitafanyiwa kazi ili kuongeza tija katika usafirishaji wa mazao yanayovunwa shambani kuingia sokoni kwa wepesi; uzalishaji wa mazao na uongezaji wa wigo wa masoko ya ndani na nje ya nchi.
“Nimepewa dhamana ya kuwa Waziri wa Kilimo na sisi ndiyo tunasimamia shibe, lishe na mlo wa Watanzania. Nina wajibu mkubwa katika kuhakikisha tunaenda kutimiza hatma ya kesho ya mtu mmoja mmoja ili wakulima na wafanyabiashara wazalishe kwa mtaji wa faida,” amesema Waziri Chongolo.
“Nimepewa dhamana ya kuwa Waziri wa Kilimo na sisi ndiyo tunasimamia shibe, lishe na mlo wa Watanzania. Nina wajibu mkubwa katika kuhakikisha tunaenda kutimiza hatma ya kesho ya mtu mmoja mmoja ili wakulima na wafanyabiashara wazalishe kwa mtaji wa faida,” amesema Waziri Chongolo.
Viongozi wengine walioshiriki katika mikutano hiyo ni pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Njombe; Mbunge wa Lupembe; Madiwani na watendaji kutoka Halmashauri ya Mji Makambako.

No comments:
Post a Comment