HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, November 10, 2025

RAIS MWINYI AZINDUA BARAZA LA 11 LA WAWAKILISHI, ATOA MWELEKEO WA SERIKALI KIPINDI CHA PILI CHA AWAMU YA NANE

 



RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amezindua rasmi Baraza la 11 la Wawakilishi Zanzibar na kutoa mwelekeo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kipindi cha pili cha Awamu ya Nane, akisisitiza dhamira ya Serikali kuendeleza maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa msingi wa amani, umoja na mshikamano wa kitaifa.

Akizungumza leo tarehe 10 Novemba 2025, katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani, Unguja, Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali itaendelea kutekeleza Ilani ya CCM 2025–2030, pamoja na ahadi za kampeni na kuendeleza mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha kwanza cha Awamu ya Nane.

Amesema Serikali itaendeleza mageuzi ya kiuchumi kwa kuimarisha sekta za uzalishaji, uwekezaji, sekta binafsi, na matumizi ya teknolojia za kisasa, ikiwa na lengo la kuongeza ukuaji wa uchumi kutoka asilimia 7 hadi 10 kwa mwaka, kudhibiti mfumko wa bei chini ya asilimia 5, kuzalisha ajira mpya 350,000, na kuongeza kipato cha mwananchi hadi Dola 1,880 kufikia mwaka 2030.

Aidha, Serikali itatekeleza ujenzi wa bandari jumuishi ya Mangapwani, bandari za abiria Mpigaduri, Kizimkazi, Shumba na Wete, pamoja na boti mbili za kisasa za mwendo kasi zitakazohudumia safari kati ya Unguja, Pemba, Tanga na Dar es Salaam.

Katika sekta ya afya, Serikali itajenga hospitali nne za mikoa, kuendeleza ujenzi wa Hospitali ya Saratani Binguni, na kuboresha Hospitali ya Mnazi Mmoja.

Katika elimu, Serikali itajenga madarasa mapya 2,000, shule tatu za sekondari za wasichana kwa kila mkoa, chuo cha kisasa cha ualimu, na kuajiri walimu 7,691.

Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali itaendelea kuimarisha utumishi wa umma kwa kuongeza mafunzo, maslahi na nidhamu ya kazi, huku taasisi za ZAECA na CAG zikiimarisha mifumo ya udhibiti wa rushwa na matumizi sahihi ya fedha za umma.

Ameongeza kuwa Afisi ya Usalama wa Shughuli za Serikali (GSO) itaongoza usimamizi wa nidhamu serikalini.

Vilevile, Serikali itajenga vituo viwili vya utamaduni Unguja na Pemba, kuendeleza michezo, na kukamilisha maandalizi ya AFCON 2027.

Akizungumzia Uchumi wa Buluu, Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali inalenga kuongeza idadi ya watalii wa kimataifa kutoka 800,000 hadi 1,500,000 kwa mwaka, na kwa Kisiwa cha Pemba watalii kuongezeka kutoka 200,000 hadi 300,000 kwa mwaka.

Ameeleza kuwa Serikali itaendeleza uvuvi na kilimo cha mwani kwa kuimarisha miundombinu ya uvuvi, ikiwemo madiko na masoko makubwa ya samaki, pamoja na kuwawezesha wafugaji wa mazao ya baharini kama samaki, matango bahari na kaa kwa njia za kibiashara.

Uzalishaji wa mwani mkavu unatarajiwa kuongezeka kutoka tani 19,715 mwaka 2024 hadi tani 40,000 mwaka 2030.

Serikali pia itaendelea kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 100, na mafunzo ya usimamizi wa fedha za ujasiriamali kwa wazalishaji na wafanyabiashara wadogo.

Aidha, Serikali itaandaa mpango maalum wa vijana wajasiriamali na wabunifu ili kukuza miradi yao na kuzalisha ajira mpya 350,000.

Dkt. Mwinyi amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kulinda ustawi wa watu wenye mahitaji maalum, wanawake, watoto na wazee, na kukamilisha ujenzi wa nyumba 4,715 katika maeneo ya Chumbuni, Nyamanzi na Kisakasaka Unguja, pamoja na maeneo mengine ya Pemba.

Katika sekta ya usafiri wa anga, Serikali imelenga kuongeza idadi ya abiria wa ndege kutoka 2,140,986 hadi 2,824,011 kwa mwaka, kujenga vituo viwili vya mafuta ya ndege, karakana ya matengenezo ya ndege, na eneo la maegesho kwa mita za mraba 106,000.

Serikali pia itaendeleza barabara ya kurukia ndege Pemba na kujenga jengo jipya la abiria.

Kwa upande wa sekta ya uzalishaji, Serikali itaanzisha sekta ya taifa ya chakula, kukarabati maghala manne na kujenga vihenge (silos) katika Dunga (Unguja) na Chamanangwe (Pemba) vyenye uwezo wa kuhifadhi tani 60,000 kwa wakati mmoja.

Serikali pia itajenga barabara kuu ikiwemo Tunguu–Makunduchi (km 48), Fumba–Kisauni (km 12), Mkoani–Chake Chake (km 43.5), na barabara za utalii Nungwi (km 12), sambamba na uwekaji wa taa za barabarani katika maeneo mbalimbali ya miji.

Baraza la Wawakilishi Zanzibar linatarajiwa kuanza rasmi shughuli zake tarehe 11 Februari 2026.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad