HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, November 20, 2025

NEMC yashiriki COP30 Brazil, Kuja na mkakati mpya za kukabiliana na tabianchi

- Ushiriki wake kuleta manufaa kwenye miradi na mazingira

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeshiriki Mkutano wa thelathini wa nchi wanachama wa Mkataba wa Kimataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC COP-30), unaoendelea jijini Bélem, nchini Brazil kuanzia tarehe 03/11/2025 na unatarajiwa kukamilika tarehe 21/11/2025.

Akiongoza ujumbe wa NEMC katika Mkutano huo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Mhandisi Mwanasha Tumbo aliyeambatana pia na Makamu Mwenyekiti, Wakili Alex G. Mgongolwa aliwataka watumishi wa Baraza kuhakikisha wanatumia vyema jukwaa la mkutano huo kupata fursa za fedha za miradi ili kuweza kuhakikisha unaleta matokeo chanya katika kutekeleza vyema nguzo ya mazingira katika Dira ya Taifa ya 2050.

Katika kutekeleza hilo, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi, ameongoza ujumbe wa NEMC kwenye Mikutano mbalimbali ya uwili ili kuimarisha ushirikiano na wadau katika sekta ya Mazingira.

Baadhi ya Mikutano hiyo ni pamoja na mkutano wa uwili na Benki ya Maendeleo ya Africa (African Development Bank), uliohusu kuanza kwa mradi uliowasilishwa na Baraza na kupitishwa na benki hiyo. Mradi huo wenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 15 unatarajiwa kutatua changamoto za mabadiliko ya tabianchi katika maeneo ya pwani yaani Dar es Salaam, Pwani na Pemba.

Aidha, Dkt. Semesi alikutana pia na Sekretarieti ya Mfuko wa Kimataifa wa kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi (Adaptation Fund-AF) ambapo aliweza kuwahimiza Adaptation Fund kukamilisha taratibu za kulipatia Baraza ithibati ya pili (reaccreditation) sambamba na kukamilisha mapitio ya miradi iliyowasilishwa yenye jumla ya thamani ya Dola za Marekani milioni 35. Katika mazungumzo hayo, mfuko wa Adaptation Fund umelihakikishia Baraza kwamba taratibu za ithibati zitakamilika ndani ya wiki chache kuelekea mwishoni mwa mwaka huu.

Hata hivyo Adaptation Fund umeidhinisha ripoti za mwaka za miradi ya SWAHAT na Bunda inayosimamiwa na Baraza Pamoja na kuachilia kiasi cha takribani Dola za Marekani laki 4 ili kukamilisha utekelezaji wa miradi hiyo.

Sambamba na hayo, Dkt. Semesi ameongoza ushiriki katika vikao mbalimbali vya kitaalam, mikutano ya pembezoni pamoja na kuanzisha mchakato wa mashirikiano na taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi ili kupanua wigo wa kujipatia fedha za kupambana na mabadiliko ya tabianchi. Baadhi ya taasisi hizo ni pamoja na Mfuko wa Kitaifa wa Maji (National Water Fund), Pew Charitable Trust, Benki ya Dunia, Global Climate Mobility, Global Methen Hub, IUCN na Ocean Vision.

Timu ya wataalam iliyoambatana na ujumbe wa Bodi kwenye Mkutano huo ni pamoja na Dkt Careen Kahangwa, Bw. Fredrick Mulinda, Bw, Paul Kalokola, Bi. Jackline Nyantori na Bw. Rahim Kantinga.




No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad